SERIKALI imemsimamisha kazi Meneja wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Moses Swai kwa kukiuka maadili ya kazi na kushindwa kushughulikia matatizo ya wafanyakazi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa baada ya wafanyakazi kugoma kupokea mapendekezo ya awali kati ya wawakilishi wa wafanyakazi, menejimenti na serikali.
Mapendekezo hayo yalihusu nyongeza ya mishahara yao na walitakiwa kuanza kulipwa Januari mwakani, pamoja na madeni ya mishahara iliyopaswa kuanza kulipwa Aprili mwaka kesho.
Mapendekezo hayo yaliyoletwa na katibu mkuu yalikataliwa na wafanyakazi hao ambao walimtaka kiongozi huyo kuondoka.
Baada ya saa nne, Katibu Mkuu Mussa alirudi kiwandani hapo akiwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda huku akiwa na marekebisha kwa baadhi ya makubaliano ambayo wafanyakazi waliyakubali na kuahidi kurudi kazini.
Katika mkutano huo wa mara ya pili, Mussa alitangaza kumsimamisha kazi Meneja wa kiwanda hicho, Swai.
Vilevile aliwaahidi wafanyakazi hao kulipwa mishahara yao kwa kiwango cha Sh 150,000 kuanzia Desemba pamoja na posho ya Sh 65,000. Pia aliahidi madai mengine yatalipwa ndani ya miezi sita.
“Natangaza kumsimamisha Swai na msiwe na wasiwasi hamtamwona tena na hatua nyingine bado zinachukuliwa. Lakini pia ongezeko la mshahara huo hautambagua mfanyakazi yeyote kwa maana kwamba wote mtalipwa kiasi hicho cha fedha kuanzia mwezi huu.
“Waziri Mkuu aliniagiza kufanya kazi ya kuvitambua viwanda ambavyo wawekezaji wake wamekuwa wababaishaji na uzalishaji wake ukiwa hauna tija ili kama ikiwezekana kuwanyang’anya viwada hivyo na kuwapa wamiliki wengine na utekelezaji wa kazi hiyo utaanza karibuni,”alisema Mussa.