MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, imetupilia mbali pingamizi lililotolewa na mawakili wa utetezi katika kesi inayomkabili Wakili Median Mwalle na wenzake watatu.
Jaji Gadi Mjemas alitoa uamuzi huo jana aliposikiliza mashahidi wa pande zote mbili baada ya kutokea mvutano wa sheria ulioibua kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kuhusiana na kupokelewa maelezo ya mshitakiwa wa nne, Elias Ndejembi.
Jaji Mjemas alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili, aliona hakukuwa na ukiukwaji wa sheria kama walivyodai mawakili wa utetezi na hivyo kuamua kutupilia mbali pingamizi hilo.
Katika kesi hiyo ndogo, mawakili wa utetezi waliiomba mahakama isipokee maelezo ya mshitakiwa wa nne kama kielelezo cha ushahidi kwa kuwa hakikuonyesha muda ambao mshitakiwa aliwekwa chini ya ulinzi.
Pingamizi la pili lilikuwa ni maelezo hayo kutoonyesha kama mke wa Ndejembi ( Imelda Ndejembi), alikuwapo wakati mume wake anahojiwa na kuandika maelezo kama ambavyo sheria inataka mtuhumiwa akiandika maelezo awe na ndugu, jamaa au wakili.
“Lalamiko la ukiukwaji wa sheria katika kipengele cha muda anaotakiwa kuhojiwa mtuhumiwa baada ya kuwekwa chini ya ulinzi halina msingi. Kwa hiyo, pingamizi hili nalitupitilia mbali,”alisema Jaji Mjemas
Baada ya kutupilia mbali hoja hizo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, uliieleza mahakama kuwa uko tayari kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo kwa kuwa umekwisha kujiandaa.
Kesi hiyo iliahirishwa jana hadi leo baada ya kuelezwa kuwa wazee wa mahakama hawakuwapo.
Katika shauri hilo, mbali na Wakili Mwale, watuhumiwa wengine ni Don Bosco Gichana ambaye yeye na Mwale wanatetewa na Omary Omary na Innocent Mwanga.
Mshitakiwa mwingine ni Boniface Mwimbwa anayetetewa na Albert Msando na Juliet Tarimo na Ndejembi anatetewa na Mosses Mahuna na Buheri Ngoseki.