25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mahiga: Vilivyoibiwa ni vipande viwili vya Kompyuta Ofisi ya DPP

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

BAADA ya kimya kutawala kwa takribani siku tatu tangu liripotiwe tukio la wizi wa kompyuta katika ofisi ya Mwendesha mashtaka, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga amejitokeza na kusema kompyuta zilizoibiwa ni za ofisi ya ndogo ya mashtaka ya Mkoa wa Dar es Salaam na si ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga.

Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari kuwa walipata taarifa za wizi huo Jumanne asubuhi ya wiki hii na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi.

Kutokana na ukimya juu ya wizi huo kuliibuka maswali mengi, kubwa lilikuwa ni lile kwanini wizi huo umetokea wakati huu ambao DPP anatekeleza ushauri wa Rais, Dk. John Magufuli  wa kusamehe watuhumiwa wa uhujumu uchumi na utakatatishaji fedha ambao wamekiri makosa na kurudisha fedha ambapo baadhi ya mafaili yao yapo ofisi ya DPP?

Aidha wapo waliokuwa wanahoji  aliyeiba au walioiba kompyuta hizo wana madhumuni gani? na je wanataka kutekeleza agenda gani?

Maswali hayo yamejibiwa kwa uchache na Dk. Mahiga jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dk. Mahiga alisema nyaraka zote za uhujumu uchumi ziko salama na ofisi ya DPP haijaguswa.

Alisema kompyuta hizo zilizoibwa katika ofisi ndogo ya mkoa  wa Dar es Salaam hazina athari zozote za kiutendaji katika ofisi hiyo.

“Nimeona vyombo vya habari mfano gazeti linasema; nyaraka muhimu zinazohusiana na watuhumiwa walioko mhakamani zimeibiwa na zimesababisha kesi hizo kuathiriwa,”alianza kueleza bila kutaja gazeti lililoandika hivyo.

“Ofisi ya DPP anayeshughukia mashtaka ya serikali haikuguswa, taarifa zote muhimu zipo, nyaraka zipo na kilichoibwa ni vipande vya kompyuta mbili lakini ofisi ya DDP yenyewe haijaguswa,”alisema Dk. Mahiga.

Alisema ofisi hiyo ya mkoa haikuwa na nyaraka za uhujumu uchumi bali inahusisha ukusanyaji wa taarifa ambazo hata hivyo hakuzitaja.

“Kwanza ni ofisi ndogo haina nyaraka, bali ni ukusanyaji wa taarifa tu iko hapo Mkwepu street na sio kompyuta zote ni vipande vya kompyuta mbili.

“Lakini taarifa zote zinazohusu uhujumu uchumi zipo kwa DPP na ofisi yake haikuguswa na shughuli zake zitaendelea ambazo ametumwa. Kazi inavyoendelea DPP itabidi apeleke taarifa kwa Rais halafu tujue tunakwendaje,” alisema.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa wahusika wa wizi huo, alisema kinachofanyika hivi sasa ni upepelezi ambao wameliachia Jeshi la Polisi waendelee nao.

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO MASHAURIANO YA KISHERIA

Mbali na hayo, awali Dk. Mahiga alieleza kuwa mwaka huu Tanzania ni mwenyeji wa mkutano wa 58 wa mwaka wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya nchi za Asia na Afrika utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21 na 25 mwaka huu.

Alisema mgeni rasmi katika mkutano ni Makamu wa Rais, Samia  Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais Magufuli.

Aidha, alisema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri, wanasheria wakuu wa serikali, wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa, mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na viongozi waandamizi wa serikali kutoka nchi wanachama 48 wa Asia na Afrika.

Alisema mkutano wa mwaka huu utajadili masuala mbalimbali ya sheria za kimataifa ikiwa ni pamoja na changamoto za kisheria zinazoyakabili mataifa wanachama.

“Sasa tutaangalia namna bora ya kushughulikia changamoto hizo ili kuwa na dunia yenye amani, usalama na utulivu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na sheria ya kimataifa ya bahari, kuvunjwa kwa sheria ya kimataifa nchini Palestina na maeneo mengine yanayoshikiliwa na nchi ya Israel na masuala mengine yanayohusiana na Palestina.

“Pia sheria ya kimataifa katika masuala ya mitandao, utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, sheria ya kimataifa katika masuala ya biashara na uwekezaji na matumizi ya sheria za njchi nje ya nchi; vikwanzo dhidi ya nchi nyingine na mengineyo,”alisema.

Alisema katika mkutano huo, Tanzania itapata fursa ya kuwasilisha mada mbalimbali zikiwemo changamoto za sheria za kimataifa katika biashara na uwekezaji, sheria ya bahari, masuala ya mtandao kimataifa.

“Pia Tanzania itawasilisha utatuzi wa migogoro na masuala mbalimbali. Kupitia mkutano huu Tanzania itapata fursa ya kubadilishana uzoefu kutoka nchi nyingine kuhusiana na masuala ya sheria za kimataifa,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles