Mwandishi wetu -Dar es Salaam
UAMUZI uliotolewa mwanzoni mwa juma hili na Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), ikitaka Serikali kuilipa benki ya Standard Chartered Hong Kong, dola za Marekani milioni 185 (Sh bilioni 425.8) kwa sababu ya kuvunjwa kwa mkataba wa benki hiyo na Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Limited (IPTL), umezidi si tu kuongeza maswali kwenye sakata la Escrow.
Mbali na kuongeza maswali, uamuzi huo pia ni kama unaonekana kuweka gizani hatima ya mmiliki mpya wa IPTL, Harbinger Singh Seth na aliyekuwa mbia mwenza kwenye kampuni hiyo, James Rugemalilara, ambao wameandika barua kwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP).
Uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa umekuja wakati ambao Seth ameandika kukiri makosa na kuomba msamaha na kurudisha fedha anazodaiwa kama ambavyo fursa hiyo ilivyotolewa kwa washitakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Kwa upande wake, Rugemalira, ameandika barua kwa DPP akimtaka amwachie huru ili aendeleze kesi zake kusaka Sh trilioni 37 anazoidai benki ya Standard Chartered ambapo akilipwa alisema Serikali itapata kodi ya Sh trilioni sita.
Uamuzi huo uliotolewa wiki hii na ICSID ambao kiwango cha deni kimeonekana kupanda kutoka kile kilichoamriwa mara ya mwisho cha dola za Marekani milioni 148 hadi kufikia dola milioni 185 na kauli ya Serikali iliyofuatia baadae kwamba itahakikisha inasimamia utawala wa sheria kwa kuona IPTL wanalipa deni lao, ndiyo iliyozidisha maswali na kuacha kiza kuhusu hatma ya Seth na Rugemalira.
Mara baada ya hukumu hiyo ya ICSID kutoka, Msemaji wa Serikali Dk. Hassan Abbas, kupitia akaunti ya mtandao wa Twitter alisema; “Nimekuwa nikiulizwa kuhusu kesi zilizoamuliwa za Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) dhidi ya Tanesco na sasa Serikali.
“Msingi wa kesi zote mdaiwa si Serikali wala Tanesco, ni deni la Benki dhidi ya IPTL walilorithi miaka mingi kutoka wakopeshaji wa Malaysia.
“Kwa muktadha huo na kisheria, Serikali na Tanesco ziliunganishwa tu kama kanuni za kisheria zinavyomruhusu mdai kuwaunganisha wahusika wengine kwenye kesi ili kuhakikisha au kupata uhakika kuwa analipwa madai yake.
“Kwa muktadha huo natumia fursa hii kuwatoa wasiwasi Watanzania, Serikali haidawi au haijawahi kukopa Standard Chartered ya Hong Kong, ila kama Baraza la Usuluhishi lilivyoamua, tutahakikisha tunasimamia utawala wa sheria kwa kuona IPTL wanalipa deni lao.”
Kauli hiyo ya Msemaji wa Serikali inafanana kabisa na ile iliyotolewa siku hiyo hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, kwamba kazi yao ni kusaidia IPTL walipe deni wanalodaiwa.
Ni kwa namna gani Rugemalira atazidai fedha hizo na ni kwa namna gani hukumu ya mahakama hiyo ya kimataifa ya ICSID itatekelezwa kwa Benki ya Standard Chartered kulipwa Sh bilioni 425.8, ni mambo ambayo yanazua mjadala na baadhi wanaona ni vigumu kubashiri mwisho wake.
Uamuzi huo wa ICSID na msimamo huo wa Serikali ambayo inaonyesha imedhamiria kuchukua tahadhari pia umeongeza maswali kwenye sakata zima la Escrow ambalo sarakasi zake zilianza tangu mwaka 1995.
Kwa sababu ya msimamo huo wa Serikali baadhi ya watu wanaona huenda huko mbele ikafufua au hata kwenda mbali zaidi ya mapendekezo yale nane yaliyowasilishwa kupitia ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyochunguza sakata la Escrow mwaka 2014.
Baadhi ya mapendekezo hayo ni pamoja na kuitaifisha mitambo hiyo ya IPTL yenye thamani ya mabilioni ya fedha.
Jana Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Agustine Mahiga, alipoulizwa juu ya hatima ya vigogo hao kama suala barua zao zitaendelea kushughulikiwa kama walivyoomba ama uamuzi wa ICSID utaathiri suala hilo, hakutaka kulijibu.
Badala yake, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Amon Mpanju, aliyekuwa ameambatana naye, alisema “namkinga waziri wangu na hilo, hayo yatamalizwa na DPP”. Hata hivyo, juhudi za kumpata DPP Biswalo Mganga jana, hazikuzaa matunda.
Hoja zilizoibuka
Uamuzi wa ICSID wa wiki hii ambao ulitoa ushindi kwa Standard Chartered (Hong Kong), ni wa pili kutolewa juu ya sakata la IPTL.
Mwingine ni ule wa Februari, 2014, ambao uliipa ushindi Tanesco ukionyesha shirika hilo walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.
Kwa uamuzi huo ilimaanisha fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti maalumu ya Tegeta Escrow, zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hata hivyo hesabu hizo hazikifanywa na fedha zote kupewa IPTL na hapo ndio mzozo mpya ukaibuka.
Kwa sasa Rugemalira na Seth wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na tangu 2017 wako ndani ambapo wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh bilioni 309.
Lakini pia suala jingine ni namna ya kupata fedha za umma ambazo Tanesco ililipa zaidi kwa IPTL na kuhifadhiwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo IPTL walilipwa huku Tanesco ikiwa haijapata kitu.
Chimbuko la IPTL
Mwaka 1995, IPTL iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Mechmar ya Malaysia kwa ubia na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited ya Tanzania, zilisaini mkataba na Tanesco wa kuzailisha megawati 100 za umeme ambao utauziwa shirika hilo la ugavi.
Katika kampuni ya IPTL, VIP Engineering and Marketing Limited ilikuwa na asilimia 30 za Mechmar asilimia 70.
Msingi wa Benki ya Standard Chartered ya kutakiwa kulipwa dola za Kimarekani milioni 185, ni mgogoro wa mkopo zaidi ya dola milioni 100 ambao kampuni iliyokuwa ikimiliki IPTL ya Mechmar iliukopa mwaka 1998 kutoka katika ubia wa mabenki ya Malaysia ili kujenga mtambo huo wa kufua umeme wa IPTL wa MW-100 eneo la Tegeta, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ushahidi unaoelezwa kuwapo katika vyombo vya kisheria, bei halisi ya deni hilo ilikuwa ni dola milioni 101.7.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa; Agosti 2005, baada kushindwa kurejesha deni hilo la IPTL lililodumu kwa muda mrefu benki ya (SCB-HK) iliingia makubaliano ya kununua mkopo wa IPTL kwa bei ya punguzo la dola za Marekani milioni 76.1 kutoka benki ya Malaysia ya Danaharta.
Chini ya makubaliano hayo, benki ya Standard Chartered ilipewa kandarasi kadhaa ikiwamo haki ya kulipwa deni la mwaka 1998, mkataba wa Utekelezaji na Hati ya Makubaliano ya Dhamana iliyosainiwa kati ya IPTL na Serikali.
Baadae kutokana na mzozo wa kibiashara ambapo Tanesco walilalamika kutozwa fedha nyingi na IPTL, mwaka 2006 akaunti maalumu ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT ili ziwekwe fedha ambazo Tanesco walipaswa kulipa IPTL wakati ambapo mzozo wao unashughulikiwa.
Mwaka 2014 fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo zilitolewa na kupewa IPTL licha ya kwamba Tanesco ilikuwa imeshinda shauri hilo ambapo fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo zilitakiwa kugawanywa sehemu iende kwa IPTL na nyingine Tanesco.
Lakini kabla ya kuondolewa fedha zilizokuwa katika akaunti ya hiyo, kampuni ya Pan Africa Power Solution Limited (PAP) chini ya Seth ilitangaza kununua hisa asilimia 70 zilizokuwa za Mechmar, hatua ambayo ilikuwa na utata, pia nyaraka za ununuzi huo zilidaiwa kuwa ni feki.
Inadaiwa pia wakati PAP ikitangaza kununua hisa hizo, IPTL ilikuwa ina fedha tasilimu dola za Marekani 250 (Sh bilioni 575) na dola za Marekani 122 (Sh bilioni 306) zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Fedha za Escrow zililipwa kwa Seth ambaye baadaye walimalizana mahakamani na Rugemalira aliyekuwa na asilimia 30 ya hisa za IPTL na kumlipa dola za Marekani milioni 75 (Sh bilioni 172), kisha Seth kuwa mmliki wa IPTL na mali zake zote ikiwamo mitambo ya kufua umeme iliyopo eneo la Tegeta.
Mwaka 2015, Standard Chartered Hong Kong, walifungua kesi ICSID, dhidi ya Serikali juu ya kukiukwa mkataba wake na IPTL ambapo uamuzi wake ndio uliotangazwa mapema wiki hii.
Rugemalira na DPP
Rugemarila aliandika barua Oktoba 4 mwaka huu, kwenda kwa DPP akiomba aachiwe huru ili aweze kushirikiana na Serikali kupata trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Cha chartered na washirika wake.
Mshtakiwa huyo ameainisha vielelezo kadhaa vyinavyoonesha benki ya Standard chartered ilivyohusika katika sakata la IPTL.
Miongoni mwa vielelezo hivyo ni gharama zilizokuwa zinatozwa na IPTL ni dola za Marekani 1.06 kwa kWh ni za chini kuliko zilizokuwa zinatozwa na Songas dola za Marekani 4.31 kwa kWh.
Kielelezo kingine ni barua ya aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu (BoT) Januari 17 mwaka huu akiomba majina ya watu waliolipwa Sh 144,947,669,844.2 zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow kati ya Julai 5, 2006 na Machi 19 mwaka 2014.
Pia katika barua yake hiyo, Rugemalira anadai, alieleza PAP kukiri kulipwa na Benki Kuu Sh 164,513,630,314.15 na dola za Marekani 22,198,544.60 na siyo Sh 309,461,300,158.27 na dola za Marekani 22,198,544,.60 kama ilivyokuwa katika hati ya mashtaka kwenye kesi ya uhujumu Uchumi namba 27/2017.
Aliambatanisha pia nakala ya barua ya BoT yenye kumbukumbu namba NC.130/170/01 iliyoandikwa Februari 18, 2018 (2019) ikiwa ni majibu ya barua yake ya Januari 19, 2019.
Kiambatanisho kingine ni cha gazeti la Financial Times la Julai 20/21 2019 lililotoa taarifa kuwa wadau wameituhumu Benki ya Standard Chattered kwa Serikali ya Marekani kwa kutoa dola bilioni 57 isivyo halali na benki hiyo ilifikia makubaliano na mamlaka za Marekani kwa kukubali kulipa faini ya dola bilioni moja.
“Iwapo nitaondolewa mashtaka yanayonikabili itaniwezesha kuendelea na kesi nilizozifungua dhidi ya Standard Charted na washirika wake ambapo nadai Sh trilioni 20 kiasi ambacho kitaiwezesha TRA kukusanya kodi kutoka kwenye hiyo fedha Sh trilioni 6,” alisema.
Makosa ya kina Rugemalira
Rugemalira na Seth wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh bilioni 309.
Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19, 2014 Dar es Salaam walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India
Katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma walitekeleza mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Seth anadaiwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 a ya usajili wa makampuni na kuonesha yeye ni mtanzania anayeishi kiwanja namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.
Baada ya kusikilizwa Maelezo hayo ya pande zote, Hakimu Shahidi aliiahirisha kesi hiyo Oktoba 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Escrow bungeni
Sakata la Escrow lilifikia tamati bungeni Novemba 2014, ambapo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilisema fedha zilizochukuliwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ni za umma.
Akihitimisha mjadala huo, aliyekuwa mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema fedha hizo ni mali ya umma na hilo limethibitishwa na ofisi nyeti za Serikali.
Zitto alizitaja ofisi hizo kuwa ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“CAG, Takukuru na TRA kwa viapo ambavyo hawatahojiwa sehemu yoyote, walikubali kwamba fedha hizo ni za wananchi, sasa anayesimama na kupinga anatoa wapi mamlaka hayo.
“Profesa Sospeter Muhongo (aliyekuwa wWaziri wa Nishati na Madini ) alipoingia katika wizara hii, alikuta Tanesco wanapata hasara ya Sh43 bilioni kwa mwaka, lakini Desemba 2012 walipata hasara ya Sh117 bilioni na mwaka 2013 walipata hasara Sh467 bilioni, hii inaonyesha miaka mitatu imepata hasara mara nne zaidi na huyu ndiyo Profesa Muhongo,” alisema Zitto.
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa PAC, marehemu Deo Filikunjombe, alisema swali la kwanza ambalo CAG aliulizwa na kamati hiyo kuwa fedha hizo ni za nani?
“Ndiyo maana sisi tulimuuliza na CAG hakupindisha na alikuwa msafi kwa hili kuwa fedha ni za umma. “CAG, Takukuru, TRA wote hawa ni watendaji wa Serikali na wamekiri kuwa ni fedha za umma, sasa nashangaa hapa mtu anasimama na kupinga,” alisema Filikunjombe.
Alisema kwa miaka 11 Tanesco walikuwa wakisema fedha ni za kwao, lakini mwaka wa 12 kikao kimoja pekee wakasema fedha si zao, hapo hakuna ukweli wowote.