Florence Sanawa
Korosho zimeanza kumiminika kwenye maghala ambapo zaidi ya tani 200 za korosho zimeshapokelewa kwenye ya maghala ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Newala &Tandahimba Cooperative Union (TANECU) kwa msimu huu wa 2019/2020.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maghala ya Tanecu, Agrofocus na Splenders Control L.t.d Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Aziza Mangosongo amesema kuwa baada ya msimu kufunguliwa amelazimika kufanya ziara hiyo ili kuona hali ya magahala na jinsi yalivyoanza kufanya makusanyo ya korosho kwa msimu huu.
“Nimetembelea baadhi ya amkos ambapo nimekuta zipo tani 400 ambazo zinatarajia kufika kwenye vyama muda si mrefu mambo yote yako vizuri na tumejipanga kwenye magunia na kuhakikisha usalama wakulima wawe makini kuleta korosho zenye ubora kwa wakati” amesema Mangasongo .
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa TANECU, Shaibu Njauka amesema kuwa wakulima wanapaswa kuwahi kupeleka korosho katika vyama vyao vya msingi ili kuwahi soko la mnada.
“Makusanyo yameanza kwa kasi kubwa tuna uwezekano wa kupata mzigo mkubwa ndani ya wiki msimu umeshungulikiwa korosho zipelekwe amkos zikiwa kwenye madaraja ili kuziwahisha soko maghala yako wazi tayari korosho za msimu uliopita hazipo sasa tunakusanya korosho mpya kwa newala na tandahimba,” amesema.