26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yawakana wanachama wake

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya wanachama wake kuhusu kile wanachokiita ni uvunjwaji wa katiba ya chama.

Wanachama hao ambao baadhi yao wamejitambulisha kuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu, juzi waliandamana hadi ofisini kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakipeleka malalamiko.

Katika malalamiko hayo wanachama hao walisema viongozi wa Chadema wamevunja katiba ya chama hicho kwa kuruhusu chama kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), bila ridhaa ya Mkutano Mkuu wala Baraza Kuu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alisema wanachama hao ni wasaliti ambao wanakivuruga chama.

Mnyika alisema madai yaliyotolewa na wanachama hao hayana msingi kwa maelezo kuwa hakuna kanuni wala kipengele chochote cha katiba kilichovunjwa.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema wanachama hao wanatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeona Ukawa ni tishio na kwamba kimeshindwa kudhibiti nguvu ya umoja huo ndani na nje ya Bunge.

Mnyika pia alisema chama chake kina ushahidi jinsi CCM inavyofadhili mchezo huo kwa lengo la kuiaminisha jamii kuwa Chadema imejiunga na Ukawa kimakosa.

Mkutano huo pia uliohudhuriwa na wanachama wa chama hicho, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Iddy Kizota.

“Orodha ya majina yao inaonyesha wapo 82 lakini katika mkutano wao waliofanya Dar es Salaam orodha inasoma wapo 32 tumefanya uchunguzi wetu tumebaini 10 kati ya hao 32 ni wanachama feki.

“Kimsingi madai yao ni ya kipuuzi tumeshangazwa na vyombo vya habari vilivyotoa nafasi kwa madai haya ya kipuuzi na kuacha kuandika mambo makubwa kama vile bajeti na masuala ya IPTL yenye maslahi kwa taifa.

“Hoja hizi zilikuwapo katika kile kilichoitwa kuwa ni mkakati wa mabadiliko ambapo chama kilichukua hatua na kuwavua nyadhifa waliohusika na wengine kufukuzwa chama.

“Wanasema viongozi wamevunja katiba kwa kuingiza chama katika UKAWA, katiba yetu inaeleza wazi kuhusu masuala ya ushirikiano.

“Uchaguzi ulifanyika mwaka 2009 kwa hiyo uongozi uliopo madarakani unamaliza muda wake 2014 mwishoni. Mbali ya hilo, Julai 18 hadi 19 kikao cha Kamati Kuu kitafanyika kupanga ratiba ya uchaguzi ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

“Ndiyo maana nasema hawa watu ni wasaliti na wengine ni mamluki. Kipo chama cha upinzani ambacho hakipo katika Ukawa kinashiriki mchezo huu.

“Pia tunayo majina ya baadhi ya viongozi wa Serikali wanaofadhili mchezo huu, leo hatuhitaji chama wala majina ya hao vigogo tumekuja hapa kujibu madai haya ya kipuuzi majina tutataja siku nyingine,” alisema.

Madai mengine yaliyotolewa na wanachama hao ni kuhusu ubadhirifu, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za chama madai ambayo Mnyika aliyapinga.

“Chadema siyo chama cha ufisadi ni sisi ndiyo tulimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akague hesabu za vyama vya siasa inakuwaje leo tuzuie taarifa zetu za fedha?

Hata hivyo Mnyika alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi kuweka hadharani ripoti za vyama vyote zinazohusiana na fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles