32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hasunga apigia chapuo ununuzi mbolea pamoja

Mwandishi wetu -Katavi

KUTOKANA na uwepo wa mfumo wa ununzi wa mbolea kwa pamoja (BPS), Serikali imeviagiza vyama vya ushirika vya msingi (Amcos) na vyama vikuu (FCU) kuanza kushiriki ununzi wa mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati.

Agizo lilitolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo kitaifa yamefanyika viwanja vya Shule ya Msingi Kashaulili, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.

Hasunga alisema kuwa ili kuongeza matumizi ya mbolea nchini, Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu, ikiwemo mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS).

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa mbolea kuuza mbolea kwa bei elekezi iliyopangwa na Serikali na wazingatie bei hizo kwa mbolea za kupandia (DAP) na kukuzia (Urea) ambazo zinaingizwa nchini kwa mfumo wa Uingizaji wa Mbolea kwa Pamoja yaani Bulk Procurement System (BPS).

“Kama mnavyofahamu, Serikali imeendelea kuratibu utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (Tanzania Agriculture Development Bank – TADB), Benki ya Uwekezaji (Tanzania Investment Bank – TIB) na Mfuko wa Pembejeo wa Taifa.

“Hivyo, nitoe wito kwa wakulima wote wa Mkoa wa Katavi na mikoa mingine kujiunga katika ushirika ili kuweza kutumia fursa zinazotolewa na taasisi hizi ili kujiletea maendeleo,” alisema Hasunga.

Alisema kuwa ili kuwa na matumizi sahihi ya mbolea, ufahamu kuhusu afya ya udongo ni muhimu, hivyo ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoa taarifa ya afya ya udongo kwa wakulima na wadau wengine ili matumizi ya mbolea yaendane na mahitaji ya zao na udongo husika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera alisema kuwa tayari Serikali imetangaza bei elekezi ya mbolea, hivyo wafanyabiashara watakaokiuka na kuanza kuuza kwa bei zaidi ya hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imedhamiria kuwanufaisha wakulima kwenye sekta ya kilimo, hivyo kukiuka maelekezo ya Serikali kwa wafanyabiashara wa mbolea hawana tofauti na wahujumu uchumi.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFRA,  Dk. Steven Ngailo, alisema mbolea ya kukuzia na kupandia tayari imewasili nchini, hivyo wakulima wana fursa mahususi ya kujitokeza na kuendeleza sekta ya kilimo katika kuongeza uzalishaji wa chakula kwa biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles