32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ampongeza RC kwa kuwacharaza viboko wanafunzi

ELIZABETH HOMBO Na ELIUD NGONDO

RAIS Dk. John Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, kwa kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya ambao walikamatwa na simu huku wakihusishwa na kuchoma mabweni ya shule hiyo.

Juzi, RC Chalamila aliwachapa viboko wanafunzi hao jambo lililozua mjadala kabla ya jana kurudi shuleni na kueleza kushangazwa na watu wanaoohoji alipopata  mamlaka ya kuwachapa wanafunzi hao.

Alisema kama mkuu wa shule anaruhusiwa kuwachama walimu, yeye pia anatakawa kuwacha zaidi kwa sababu ndiye bosi wa wakuu wa shule walio kwenye mkoa wake.

Akiwa shuleni hapo pia, aliagiza wanafunzi 392 wa kidato cha tano na sita kurudi nyumbani hadi Oktoba 18 ambapo watatakiwa kurejea shuleni wakiwa na Sh 200,000 kila mmoja ambazo zitakarabati mabweni hayo.

Pia wanafunzi 14 waliochapwa na RC huyo baada ya kukutwa na simu, wao aliwataka kurudi shuleni siku hiyo wakiwa na Sh 500,000 kila mmoja huku wakiwa wameambatana na wazazi wao.

JPM apigilia msumari

Akizungumza jana katika ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe, Rais Magufuli kuna haja ya kufanyiwa marekebisho sheria inayozuia adhabu hiyo kwa sababu viboko vinafundisha watoto.

“Leo nilikuwa naongea na mkuu wa mkoa wa Mbeya nikamwambia nakupongeza sana kwa kuwatandika wale wanafunzi, nikamwambia umewatandika viboko vichache, nikamwambia hawa watoto wote fukuza na bodi ivunjwe kwa sababu pia ni uzembe wa bodi.

“Wengine wanasema eti haki za binadamu! Haki za binadamu watoto wawe na viburi vya kipumbavu hivi, ni lazima ifike mahali tuache mambo ya mchezo katika mambo ya maendeleo, hizi fedha zimechangwa na wazazi masikini.

“Kwamba watoto wetu wasome, unamnyang’anya mwanafunzi simu halafu anachoma jengo? Nidhamu ya namna gani hii? Hao wa haki za binadamu wakayajenge basi hayo mabweni, kurudi hao watoto lazima baba zao walipe ili mabweni yale yajengwe na wale waliohusika kabisa peleka jela.

“Ndugu zangu nayasema haya sio kwamba sina huruma, mimi nina upendo mkubwa tena nilikuwa mwalimu ninafahamu, ninawaomba wazazi na viongozi muache haya mambo kwamba akichapwa viboko nafikrii kama kuna mahali tumekosea ile sheria ikafanyiwe marekebisho wawe wanatandikwa viboko.

“Eti mkuu wa mkoa ametandika viboko maana yake nini hata Ulaya wanachapa viboko mimi nimeishi Ulaya, kiboko kinafundisha na ndio maana watoto wanakuja nyumbani hasomi, amekula mtepesho baba anasema huu ndio usomi, tandika viboko hata nyumbani,”alisema.

Alisema bila kuwachapa watoto taifa litaharibika hivyo lazima kuwe na vijana wenye nidhamu na maadili.

“Kwahiyo nimempongeza yule mkuu wa mkoa, nimempongeza sana kwa hiyo wakuu wa mikoa tandika viboko kwa sababu haiwezekani.

“Wewe Silinde (David- Mbunge wa Momba) shule uliyosoma hukuchapwa viboko? Ulipigwa viboko ndio maana umefika mpaka ubunge na ndio maana hata bungeni hutukani CCM kwa sababu unaona inatekeza ilani ya uchaguzi.

“Na mimi nakupongeza sana umewakilisha vyema Bunge la Afrika na walikupigia kura hata wabunge wa CCM, nafahamu majimbo mengine tunayapoteza sisi CCM wenyewe, wakati ule mmepigana vita huyu kijana akapenya kule angalia hata sura yake haifananii kule inafanana kwenye rangi ya kijani,”alisema.

RC

Jana asubuhi akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo, RC Chalamika alitoa muda wa saa nne kuanzia  1:00 hadi saa 4:00 asubuhi kwa wanafunzi hao kufungasha kila kilicho chao na kuondoka shuleni hapo.

Chalamila aliiwataka kurejea Oktoba 18, wakiwa wamelipa fedha hizo kupitia akaunti ya shule wakiwa pia na barua ya kukiri makosa yao na kuahidi kutorudia.

 “Tumeamua tunafunga kidato cha tano na Sita kwa sababu hakuna sehemu ya kulala, mabweni mliyokuwa mkilala ndiyo mmeyachoma moto,”alisema Chalamila.

Chalamila alisisitiza kuwa wanafunzi wote wanatakiwa kurejea shuleni Oktoba 18,  huku akionya yeyote atakayekaidi Serikali itamfuata aliko na kumkamata.

Alisema hata kama mwanafunzi ambaye hatalipa fedha hizo akihamia shule za binafsi, atafuatwa huko na kuzuiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha sita akiwa popote ndani ya mipaka ya Tanzania.

Alisema walimu waliokuwa wakifundisha kidato cha sita pia wanapewa mapumziko kwa kipindi hicho ambacho wanafunzi watakuwa nyumbani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi, aliwaasa wanafunzi hao kutekeleza maagizo yote waliyopewa ili waendelee kupata haki yao ya elimu.

Alisema kukaidi kutekeleza maagizo hayo kutasababisha wafukuzwe shule na kuzuiwa kufanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mahali popote nchini.

“Maelekezo hayo hakikisheni mnayafanyia kazi kadri mnavyopewa, nje ya hapo mtajipotezea haki ya kusoma katika maisha yenu,”alisema Mahundi.

Baadhi ya wanafunzi walisema uamuzi huo unazidi kuwaongezea machungu kwa vile baadhi yao waliunguliwa na vitu vyao ndani ya mabweni na hawana namna ya kupata nauli za kurejea majumbani mwao.

Mmoja wa wanafunzi hao, Masunga Genge ambaye anasoma kidato cha sita, alisema ametokea mkoani Simiyu na wazazi wake hawajui lolote kuhusiana na mikasa iliyowapata na hana uwezo wa kusafiri ingawa anatakiwa kuondoka shuleni hapo.

Septemba 30, mabweni ya shule ya Sekondari Kiwanja yaliteketea kwa moto, tukio ambalo linahusishwa na wanafunzi wa shule hiyo ambao siku hiyo mchana walipekuliwa na kunyang’anywa simu na walimu wao.

JPM na ziara yake

Rais Magufuli ambaye yupo katika ziara ya siku tatu mkoani Songwe kukagua miradi ya maendeleo, awali akizungumza na wananchi wa eneo la Mahenge, alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwangela kufanya uchunguzi wa fedha wanazochanga wananchi kwa ajili ya shule za msingi kata ya Myovizi wilayani Mbozi.

Kiongozi huyo wa nchi, alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa eneo hilo la Mahenge kulalamikia wingi wa michango ukiwamo wa Sh 25,000 hivyo aliagiza kiasi hicho cha fedha kutochangwa tena.

“Mkuu wa mkoa uje kufuatilia fedha zote zilizochangwa kwa wananchi, hawawezi kuchangishwa fedha zote hizi, ningekuwa mbunge nisingeruhusu wananchi wachangishwe,”alisema Rais Magufuli ambaye alitoa Sh milioni 5.

Awali, Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga alisema michango inayochangishwa kwenye jimbo hilo inaasisiwa na ofisi ya wilaya.

Haonga alisema amekuwa akisoma mapato na matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo ambazo hupelekwa katika miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa madarasa na zahanati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles