AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM
Hospitali ya Mloganzila kwa mara ya kwanza itoa huduma ya kibingwa kwa kufanya upasuaji wa kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia ambapo takribani watoto watatu wamepata huduma hiyo.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dk Julieth Magandi amesema aina hiyo ya upandikizaji imekuwa sehemu ya mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa kwa hospitali hiyo.
“Jana Alhamisi Oktoba 3, tumetimiza mwaka mmoja wa kusimamia hospitali hii iliyowekwa chini ya uangalizi na usimamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzia Oktoba 3, mwaka jana.
“Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imejengewa uwezo na kuanza kufanya upasuaji mkubwa wa kupandikiza watoto watatu vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant) hivyo kufanya idadi ya waliopandikizwa kufikia 34 tangu kuanzishwa huduma hiyo nchini Juni, mwaka juzi,”
“Hatua hii inaifanya Hospitali ya Mloganzila kuimarika katika utoaji huduma za kibingwa nchini,” amesema Dk Magandi.