Magufuli ampongeza RC Mbeya kwa kutandika viboko wanafunzi

0
790

Anna Potinus

Rais John Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kitendo alichokifanya cha kuwatandika viboko wanafunzi zaidi ya 13 wa Shule ya Sekondari ya Kiwanja ya mkoani Chunya baada ya kubaini wanamiliki simu wakiwa shuleni kitendo ambacho ni kinyume na taratibu za shule hiyo.

Ametoa pongezi hizo leo Ijumaa Septemba 4, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Songwe katika ziara yake ya kikazi ya siku nne ambayo ameanza rasmi leo kwa kukagua na kuzindua kiwanda cha kukoboa kahawa cha GDH na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa huduma za maji katika mji wa Vwawa.

“Ifike mahali tunapozungumzia maendeleo ni maendeleo kweli, leo nilikuwa naongea na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na nimempongeza kwa kuwatandika viboko wale wanafunzi nikamwambia uliwatandika vichache haiwezekani serikali tunatoa mabilioni kwaajili ya kujenga madarasa na shule halafu mtoto anaenda kuichoma nikawaambia awafukuze wote kwahiyo form five na form six wote wamefukuzwa na bodi imevunjwa kwasababu ule ni uzembe wa bodi ya shule hiyo,”

“Ni lazima tufike mahali tuache mambo ya mchezo katika maendeleo hizi fedha zimechangiwa na wazazi masikini halafu unaenda na simu shule ukinyang’anywa unachoma jengo hii ni nidhamu ya namna gani hao wa haki za binadamu wakajenge basi hayo mabweni na nimesema kurudi hao watoto ni lazima baba zao walipe ili mabweni hayo yajengwe na hao wengine waliohusika peleka wote jela,”

“Ninayasema haya sio kwamba sina huruma mimi nina upendo mkubwa tena mimi nimeshakuwa mwalimu ninafahamu na ninawaomba wazazi na viongozi muache haya mambo ya kusema ukipigwa viboko tena nafikiri mahali tulipokosea ile sheria ikafanyiwe marekebisho wawe wanatandikwa viboko hata Ulaya wanatandikwa viboko mimi nimekaa huko kuna shule ambazo wanazisomea wao wanatandikwa lakini shule ambazo wanataka wavuta bangi hawatandikwi, kiboko kinafundisha,” amesema rais Magufuli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here