Mwandishi wetu
TIMU ya Taifa, Taifa Stars, inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda, mchezo utakaochezwa Oktoba 14 mwaka huu, ugenini mjini Kigali.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kigali, ni wa kalenda ya FIFA.
Kwa mujubu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, Shirikisho la Soka Rwanda na TFF wamefikia makubaliano yote muhimu ya mchezo huo.
Kwa upande mwingine, waamuzi kutoka nchini Burundi watachezesha mchezo wa marudiano wa Chan kati ya Stars na Sudan, utakaopigwa kwenye Uwanja wa El Merriekh, mjini Omdurman.
Mwamuzi wa katikati ni Thiery Nkurunzinza ambaye atasaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja, Willy Habimana, mwamuzi msaidizi namba mbili ni Shabani Nitungeko na mwamuzi wa akiba ni George Gatogato.
Tyaari kikosi cha wachezaji 28 wa Stars kimeitwa na Kaimu Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije kujiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda.
Kati ya wachezaji hao, yupo beki walia, Shomari Kapombe ambaye awali aliachwa kutokana na kukabiliwa na majeruhi.
Kikosi kamili kilichotangazwa jana kinaundwa na Juma Kaseja, Metacha Mnata, Said Kipao, Salum Kimenya, Kapombe, Gadiel Michael, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kelvin Yondan, Erasto Nyoni, Bakari Nondo, Himid Mao, Jonas Mkude, Kelvin John na Farid Mussa.
Wengine ni Adi Yusuph, Idd Seleman, Mudathir Yahya, Salum Abubakar, Frank Domayo, Mzamiru Yasin, Shaban Idd, Ayoub Lyanga, Abdulaziz Makame, Andrew Simchimba, Miraji Athuman, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mbwana Samatta na Simon Msuva.