Theresia Gasper-Dar es salaam
KOCHA msaidizi wa timu ya Azam, Iddy Cheche, ameweka wazi kuwa bado hawajakata tamaa na wameanza mazoezi kujiandaa na mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Triangle United, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 29, mwaka huu nchini Zimbabwe.
Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa nyumbani wa Azam Complex uliopo Dar es Salaam, ni wageni Triangle United ambao walifanikiwa kuondoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Cheche alisema wameanza mazoezi kwa nguvu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwani hawapo tayari hali hiyo ijirudie mechi ya marudiano.
“Baada ya mchezo wa kwanza tuliwapa mapumziko ya siku mbili wachezaji wetu. Wamesharejea na tumeanza mazoezi rasmi kujiandaa kupata matokeo ugenini,” alisema Cheche.
Alisema hawawezi kukata tamaa zaidi ya kupambana kwani matokeo yanapatikana uwanja wowote iwe ugenini au nyumbani.
Cheche alisema kwa sasa wataangalia zaidi yale makosa yaliyojitokeza nyuma ili yasijirudie katika mchezo ujao.