ANDREW MSECHU
VIONGOZI wastaafu wa Tanzania wamekuwa kivutio katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kisini mwa Afrika (SADC) ulioanza jana jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wastaafu waliohuduria mkutano huo ni marais wa awamu tatu zilizopita, ambao ni Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Pia katika mkutano huo, alikuwepo pia Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume na aliyekuwa makamu wa Rais wa Tanzania Dk Gharib Bilal.
Wastaafu wegine waliohudhuria mkutano huo ni waliokuwa mawaziri wakuu, ambao ni Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba na John Malecela, na waliowahi kuwa wakuu wa majeshi, Davis Mwamunyange na George Waitara.
Katika mkutano huo ambao Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa SADC kwa mwaka mmoja.
Akizungumzia uwepo wa viongozi hao, mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake rasmi jana, Rais Dk Hage Geingob wa Namibia, alisema Tanzania inaonyesha mfano wa kuvutia unaostahili kuigwa, hasa kutokana na kuwaona viongozi hao katika mkutano huo.
“Ninawaona viongozi, marais wastaafu wote wamekaa pamoja nasi katika mkutano huu, ninajivunia sana utamaduni huu wa Watanzania. Mnaonyesha mfano wa kipekee hasa kwa namna mnavyoendesha mambo yenu, ni heshima ya kipekee kwetu,” alisema.
Alisema miongoni mwa mambo atakayoyakumbuka maishani ni mchango wa Serikali ya Tanzania alipokuwa kijana mdogo, wakati huo akiwa mwanaharakati wa chama cha Ukombozi cha Namibia cha SWAPO, hasa kwa malezi aliyoyapata akiwa nchini.
Alisema wakati huo, hatasahau mchango wa Malecela, ambaye alikabidhiwa kwake kama mlezi na mkufunzi, kwa jinsi alivyomfundisha namna ya kuwa imara na jasiri, hatua iliyomjenga na kumfanya kuwa miongoni mwa viongozi wa kutumainiwa wa SWAPO.
“Nimefurahi, hapa ninapoangalia ninamuona aliyekuwa mkufunzi (mentor) wangu, mzee Malecela ambaye nilikabidhiwa kwake nikiwa kijana mdogo, nikitokea SWAPO, alinilea vyema. Kuna wakati niliwahi kupata kashkash, nikamtumia ujumbe, akaja kuninusuru na akanitania lakini akinifunza, kuwa niache mambo yangu ya ujana,” alisema.
Alisemsa japokuwa Mwalimu Julius Nyerere alishatangulia mbele za haki miaka 20 iliyopita, kutokuwepo kwake moja kwa moja katika mkutano huo, kunawakilishwa na mafundisho yake ambayo yameendelea kuwajenga katika utendaji wao, hasa kuimarisha mjumuiko ndani ya SADC ambayo aliiasisi.