Derick Milton – Simiyu.
Asasi isiyo ya kiserikali inayotoa msaada wa kisheria (LSF), imesema kuwa Migogoro mingi ya ardhi , kanda ya ziwa inatokana na wanaukoo kutoelewana ambapo waathirika wakubwa ni wanawake, vijana na watoto.
Aidha wanawake wengi hawanufaiki na umiliki wa ardhi badala yake hati miliki imekuwa ikibaki kwa wanaume pekee huku uelewa wa hati miliki katika maeneo ya vijijini ukiwa ni mdogo.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 5, na Mkurugenzi wa asasi hiyo ambaye pia ni Wakili wa kujitegemea, Scholastica Jullu, wakati akiongea na Mtanzania Digital kwenye maonyesho ya sikuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu.
Jullu amesema wao kama watoa msaada wa kisheria kazi yao ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya sheria katika kupunguza matatizo ya mirathi ,ndoa na migogoro ya ardhi ambayo kwa kanda ya ziwa imeongezeka.
“matatizo mengi ambayo tumekuwa tukiyapokea wanawake wanadhulumiwa mali zao hata kama walizitafuta na wenzi wao inapotokea marehemu amefariki na kuacha ardhi aliyokuwa akiitumia na familia yake wanaukoo huiondosha familia na kujinufaisha wao” amesema Jullu.
Ameongeza kuwa wamekuwa wakipokea matatizo mengi yanayohitaji msaada wa kisheria ikiwemo masuala ya migogoro ya ardhi ,taratibu na umiliki wa ardhi pamoja na matumizi yake na kueleza kuwa iwapo watawatumia wasimamizi wa kisheria watanufaika.