25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Uzazi wa mpango Afrika na ongezeko idadi ya watu

Mwandishi wetu

JAMII nyingi za Kiafrika, kupata watoto ni jambo linalochukuliwa kuwa baraka. Baadhi ya jamii huamini kuwa na watoto wengi ni ishara ya utajiri na fahari kwao.

Nchini Ghana, wenyeji wa kiasili wa Mji Mkuu wa Accra ni kabila la Ga, ambako wao mwanamke anapojifungua mtoto wake wa 10 huzawadiwa kondoo mzima. Desturi hii huitwa nyongmato.

Ukizunguka Jijini Accra leo, kwenye benki, vyombo vya usafiri, mitaani na kwengineko ni nadra kukutana na mama mwenye watoto zaidi ya wanne. Inawezekana Accra si sehemu sahihi tena ya kutafuta familia yenye watoto 10 na kuendelea.

Uzazi holea na ongezeko kubwa la watu vinatajwa kuwa chanzo cha umasikini barani Afrika.

Wakati inapata Uhuru mwaka 1957, nchi ya Ghana ilikuwa na watu milioni tano, leo hii kuna watu milioni 30. Wakati nchi ya Norway katika kipindi hicho hicho wametoka kuwa na watu milioni 3.5 hadi kufikia milioni 5.3.

AFRIKA MASHARIKI

Kinachoendelea Ghana kinaakisi sehemu nyingine za Afrika ikiwamo ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) idadi ya watu imeongezeka mara mbili nchini Kenya katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Idadi ya watu nchini Kenya hivi sasa inafikia milioni 50.9, ambapo UN wanaonya kuwa kama hatua stahiki hazitachukuliwa, basi ongezeko hilo litapaa kwa watu milioni moja kila mwaka na nchi hiyo itafikisha idadi ya raia milioni 90 kufikia mwaka 2051.

Kama ilivyo kwa Ghana, Kenya pia inapambana na umasikini unaoathiri watu wengi. Takwimu zinonesha kuwa takribani asilimia 50 ya Wakenya wanaishi katika lindi la umasikini.

HALI ILIVYO TANZANIA

Takwimu rasmi za Serikali zilizotolewa Februari mwaka jana, zinaonesha kuwa Tanzania ina watu takribani milioni 54, na ongezeko la watu linakadiriwa kufikia milioni 1.6 kila mwaka.

Licha ya wingi huo wa watu, Rais Dk. John Magufuli, aliwahi kuwahamasisha watu wanedelee kuzaa kwa sababu elimu ni bure.

Alisema wananchi wasiogope kuzaa huku akitumia msemo wa ‘fyatueni tu’ na serikali itawasomesha.

Hata hivyo kauli hiyo baadae ilikuja kutafsiriwa kuwa ni utani wa Rais aliokuwa akiwafanyia watani zake wa Kabila la Wazaramo, ambao ni wenyeji wa Jiji la Dar es Salaam.

Katika kupambana na ongezeko kubwa la watu, Kenya wamefanikiwa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo kwa sasa asilimia 53 ya wanandoa walikuwa wakitumia uzazi wa mpango kufikia mwaka 2014 kutoka asilimia 39 mwaka 2008/2009.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikihamasisha matumizi ya uzazi wa mpango ambapo imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili hiyo.

Nchini Ghana, katika jitihada za kudhibiti ongezeko kubwa la watu, mwaka jana, Mkurugenzi wa Baraza la Idadi ya Watu, Dk. Leticia Adelaide Appiah, aliwahi kupendekeza kuwekwa kikomo cha uzazi kwa kila mwanamke kuwa watoto watatu. Na ikitokea mtu akaongeza basi adhabu yake iwe kutopata msaada wowote kutoka serikalini.

UHABA WA DAWA WACHANGIA KUONGEZEKA IDADI YA WATU UGANDA

TORGOVNIK

Sasa hivi nchini Uganda kuna uhaba wa dawa za kupanga uzazi na kuzuia ujauzito.

Wakuu wa afya na asasi za kijamii wanahofu kwamba sasa wanawake na wasichana walio katika balehe wanaweza kushika mimba bila mpangilio.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), kizazi cha Uganda hadi kufikia mwaka huu, kinakaribia watu milioni 46, ambapo watu huongezeka kwa zaidi ya asilimia tatu kila mwaka.

Uhaba wa dawa za uzazi wa mpango ni tishio kwa uzazi holela, mfumo wa afya pia kwa uchumi wa nchi.

Tangu Mei mwaka huu, dawa kadhaa za kuzuia mimba, zikiwamo Sayana, ya kujipiga sindano; Jadelle na Implanon, za kupandikiza; na vidonge vya dharura, zimeadimika nchini Uganda.

Ofisa wa Wizara ya Afya, Dk. Placid Mihayo, anakiri na kuwapo kwa upungufu wa dawa hizo.

Sababu za upungufu wa dawa hizo inatajwa kuwa ni fedha, ambapo kuna pengo kubwa chini ya makisio ya Wizara ya Afya ambayo inalipia nusu tu ya dawa zinazohitajika nchini, na hivyo kutoa wito kwa wabia kuasaidia kuondokana na tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa asasi moja ya kijamii ya Coalition of Health Promotion and Social Development (HEPS-Uganda), Dennis Kibira anasema: “Kitu cha kwanza kabisa, ni mimba ziso-kusudiwa. Ukiwa na mimba isiyotarajiwa ina maana hautafikia lengo la maendeleo ya milenia, la kupunguza vifo vya wajawazito kwa thuluthi mbili; na dawa za uzazi wa mpango ndio njia mojawapo ya kufanikisha hilo.

“Upungufu wa kingamimba unamaanisha kwamba mimba zisizotarajiwa zitaendelea kuwapo na hivyo kuugharimu uchumi wa nchi.”

Zaidi ya asilimia 75 ya watu milioni 45 wanaishi vijijini nchini Uganda, wengi wao wakiwa ni wanawake wa marika ya kuweza kubeba ujauzito. Hivyo, wanahitaji dawa hizo.

“Ili kupata dawa hizo itawalazimu kulipa, na unajua matumizi kutoka mfukoni ni ghari mno nchini Uganda. Hivyo, wakazi wengi wa vijijini wanaohitaji dawa hizo huzikosa,” anaeleza Kibira.

Mseto wa HEPS-Uganda unafanya kazi katika wilaya 16 nchini humo, katika miradi ya afya ikiwamo uzazi wa mpango.

TAKWIMU ZA WHO

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani wanawake 830 hufariki kutokana na sababu zinazoweza kuepukika zinazohusha ujauzito na kujifungua. Hii yote inatokana na gharama kubwa za kupata hudumu za afya.

Asilimia 99 ya vifo hivyo vyote hutokea katika mataifa yanayoendelea.

VIFO AFRIKA MASHARIKI

Nchini Kenya kuna kiwango kikubwa cha vifo vya wajawazito. Kutokana na hilo, Serikali iliidhinisha sera ya utoaji huduma bure kwa kina mama wanaojifungua katika taasisi za umma tangu Juni 2013.

Sera hii imekuwa ikiwawezesha wajawazito kuhudumiwa bure wakati wa kujifungua katika vituo vya afya vya umma.

Mpango uliopo ni kwamba vituo hivyo vya afya hutoa huduma bure na baadaye serikali inavilipa kupitia Wizara ya Afya kulingana na idadi ya kina mama waliozalishwa.

Pia hakuna malipo yanayotolewa kwa huduma za kabla na baada ya kujifungua kwa kina mama na watoto wa hadi wiki sita.

Licha ya huduma hiyo ya bure, kiwango cha hudumu zinazotolewa bado kinazua maswali mengi huku baadhi ya wazazi katika hospitali hizo za umma wakiishia kujifungua katika hali duni na wengine hata kuishia kulala kitanda kimoja na wazazi wenzao.

Kwa upande wa Uganda, suala moja kubwa linalohusiana na afya ya uzazi ni nafasi ya kina mama kuzifikia huduma za dharura na za kiwango bora za uzazi.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi zinazoendelea, Uganda inashuhudia kiwango kikubwa cha vifo vya kina mama wakati wa kujifungua, jambo linalodhihirisha hali mbaya ya ufikiwaji wa huduma hizo za afya.

Hata wakati huduma hizo zinapopatikana, kwa kawaida idadi ya wahudumu, dawa na vifaa hospitalini inakuwa ndogo ikilinganishwa na idadi ya kina mama wanaohitaji hudumu hiyo.

Mwongozo uliotolewa na WHO ni kwamba mkunga mmoja anastahili kuwazalisha takribani wanawake 175 kwa mwaka, lakini wakunga nchini Uganda huwazalisha kati ya kina mama 350 hadi 500 kwa mwaka.

Upungufu na usambazaji mbovu wa wahudumu wa afya unaathiri kwa ujumla gharama ya huduma ya afya kwa wajawazito na watoto.

Nchini Tanzania, idadi ya wanawake wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua ni 454 kati ya 100,000. Takiwmu hizi ni miongoni mwa zilizo juu duniani.

Licha ya Serikali kupambana kumaliza tatizo hilo, hali bado si nzuri kama inavyotarajiwa.

Aidha, zaidi ya asilimia 70 ya idadi jumla ya raia nchini wanaoishi katika maeneo ya mashamabani wanashindwa kuzifikia huduma za afya ipasavyo.

Kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Magonjwa katika Maeneo ya Joto na Afya ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Heidelberg, Ujerumani, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS), wazazi wanaopokea huduma hizo hugharamia malazi, dawa pamoja na usafiri.

Usafiri pekee hugharimu nusu ya gharama nzima ya matibabu. Malipo yasiyo rasmi hayajumuishwi katika hesabu na gharama nzima hutegemea huduma inayotolewa kutoka taasisi hadi taasisi.

Kwa upande wa Kongo; licha ya ufadhili wa kimataifa, kiwango cha huduma za uzazi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imezongwa na miongo kadhaa ya vita vya kiraia pamoja na kudorora kwa hali za kijamii, kiuchumi na miundombinu duni.

Kwa mujibu wa makadirio ya serikali ya nchi hiyo ya hivi karibuni, takribani asilimia 40 ya kina mama waliojifungua mjini Kinshasa hawakujifungua katika hospitali za umma, hali inayoashiria kuwa kiwango fulani walipata huduma hizo katika taasisi zisizo chini ya Wizara ya Afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles