29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto njiti hatarini kupata matatizo ya kutosikia

Aveline Kitomary -Dar es salaam

MKUU wa idara ya magonjwa ya masikio, pua na koo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, Dk. Edwin Liyombo, amesema watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti), wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kusikia.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya matibabu ya siku tatu.

Dk. Liyombo alisema watoto wenye manjano pia wako katika kundi hatari la tatizo hilo.

“Tunafanya upasuaji wa kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia kwa wale wenye matatizo ya kusikia kwa kiwango cha juu, lakini watoto ndio waathirika na matatizo ya kusikia, hasa wale watoto wanaozaliwa ‘premature’ (njiti) na wanaozaliwa na manjano wapo kwenye hatari zaidi,” alisema Dk. Liyombo.

Alisema wakati mwingine matatizo ya kusikia kwa watoto yanatokea kwa sehemu tofauti, ikiwa ni mtoto kuzaliwa na ulemavu au matumizi mabaya ya dawa kwa mama mwenye mimba.

“Hakuna data za nchi, ila takwimu za kidunia zinaonesha kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa, kati yao watoto wanne mpaka sita wana tatizo hilo.

“Kuna sababu nyingi ambazo ni ulemavu, matatizo ya uzazi au mjamzito akitumia madawa vibaya yanaweza kusababisha matatizo kwa watoto,” alieleza Dk. Liyombo.

Alisema hadi sasa hakuna takwimu sahihi, lakini matatizo hayo yapo kwa kiasi kikubwa ambapo hadi sasa wamewapatia huduma watu 24.

“Matatizo yapo kwa kiwango kikubwa, toka mwaka 2012 hadi 2016 Serikali ilipeleka watu takribani 50 na kupata matibabu nje, gharama ni Sh milioni 60 hadi 100 na matibabu ni kwa miezi mitatu.

“Kwa wiki hii tutaweza kufikia wagonjwa 30 ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya waliofanyiwa kwa miaka 14 iliyopita kwa kuwapeleka India na sasa gharama zimepungua hadi Sh milioni 35,” alisema Dk. Liyombo.

Alisema katika kambi hiyo ya siku tatu, wanatarajia kufanya upasuaji kwa watoto nane na mtu mzima mmoja kwa kushirikiana na madaktari kutoka Misri.

“Tunaowafanyia wengi ni watoto wadogo katika kambi hii ya siku tatu, watoto wako nane na mtu mzima mmoja, ambao jumla ni tisa na wote tumewaandaa kwa miezi sita,” alisema.

Alisema matumizi ya dawa za Kwinini yasiyo sahihi husababisha watu wazima kupata tatizo la kusikia na kelele nyingi.

“Kwa wakubwa madawa ya kwinini kama dawa za malaria, kifua kikuu, ARB visipotumiwa vizuri zinaweza kupelekea matatizo ya kusikia na pia kelele nyingi, mfano disko wale madj na wanaovaa ‘ear-phone’ wanaweza kupata tatizo la kusikia,” alisema Dk. Liyombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles