Ramadhan Hassan -Dodoma
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema kati ya wanawake 10 wenye umri wa miaka 15 hadi 45, wanne wamefanyiwa ukatili wa vipigo au ngono katika maisha yao.
Takwimu hizo alizitoa jana jijini hapa wakati akizindua mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko.
Samia alisema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kupitia taarifa ya Tanzania na idadi ya watu na afya ya mwaka 2015/16, inakadiriwa kuwa kati ya wanawake 10 wenye umri wa miaka 15 hadi 45, wanne wamefanyiwa ukatili wa vipigo au kingono katika kipindi cha maisha yao.
Alisema kuwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto unahusisha vitendo mbalimbali vinavyowadhuru kimwili, kisaikolojia na kiuchumi, ikiwemo ubakaji, vipigo, matusi na kunyimwa haki za kumiliki mali.
Samia alisema takwimu hizo zinaonyesha wazi kuwa tatizo hilo bado ni kubwa na siyo la kufumbiwa macho na linahitaji utatuzi wa haraka na makini kwakuwa wahanga wengi hupata athari, kisaikolojia, kiafya na kiuchumi na hivyo kuchangia kudhoofisha maendeleo ya mhusika na jamii kwa ujumla.
“Takwimu hizi ni muhimu kwa Serikali kwenye kupanga mikakati yake ya kitaifa hususan katika kumkomboa mwananchi na changamoto mbalimbali pamoja na kumwezesha kuondokana na umasikini, Serikali tayari imeandaa mpango kazi wa miaka mitano ambao unahusisha wadau mbalimbali.
“Dhima yetu ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa kati utakaojengwa kwa uchumi wa viwanda, ni wazi kuwa viwanda hivi havihitaji tu malighafi, lakini pia nguvu kazi yenye afya na tija katika sekta zote za mnyororo wa thamani ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea.
“Suala la kutumia lugha chafu, kuwashika maungo pamoja na vitendo vya kiudhalilishaji dhidi ya wanawake ni udhalilishaji usiokubalika, wanawake na wanaume wote wana nafasi sawa katika nchi yetu na haki hizi zinalindwa na katiba yetu.
“Kwa muktadha huo basi ni lazima tujenge utamaduni wa kuheshimiana wanawake na wanaume na hivyo kuondokana na taratibu zinazodhalilisha wanawake na kupunguza nguvukazi na tija katika uzalishaji mali,” alisema Samia.
Pia alisema kuwa vitendo vya rushwa, kudhalilisha utu wa wanawake, utu wa mtu, kumdhalilisha mtu kimwili, kumpiga ni kosa kulingana na sheria za nchi na hivyo ni wajibu wa wanajamii kutii sheria za nchi.
Akizungumzia vituo vya mkono kwa mkono vya kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia vilivyoanzishwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano, alisema vimeongezeka kutoka vinne kwa mwaka 2015/16 hadi kufikia 13 kwa mwaka 2018/19 na kwamba vimeanzishwa katika mikoa sita ya Tanzania bara, ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Mbeya, Iringa na Shinyanga.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alimpongeza Jaji Mkuu Tanzania, Profesa Ibarahim Juma kwa kutoa waraka wa maelekezo ya ukomo wa usikilizwaji wa kesi za ukatili wa kijinsia kwa wanawake, wazee na watoto kuwa ndani ya miezi sita, na kama itabidi kutokana na sababu mbalimbali iwe miezi tisa.
“Hilo ni jambo kubwa na anaonyesha namna gani anavyotambua na kujali changamoto zinazoyakabili makundi hayo hapa nchini,” alisem Ummy.