NYOTA wa klabu ya Arsenal, Alexis Sanchez na Mesut Ozil wanatarajiwa kuongezewa mikataba mipya ambayo itawafanya wachezaji hao kukaa kwa muda mrefu katika klabu hiyo.
Klabu hiyo tayari imeanza mazungumzo na Sanchez, ambapo mchezaji huyo ameonekana kukubali kuongeza mkataba wa miaka mitano kwa kitita cha pauni 155,000 kwa wiki.
Katika mkataba wake wa sasa, Sanchez anachukua kitita cha pauni 130,000 kwa wiki, lakini mkataba huo utamfanya aongeze kitita cha pauni 25,000 na kumfanya avune jumla ya pauni 155,000 kwa wiki.
Kwa upande wa Ozil, mazungumzo yanakwenda vizuri na yanatarajia kukamilika wiki ijayo, huku ikiwa mchezaji huyo anaongoza kwa mshahara mkubwa kwa wiki ambapo anachukua kiasi cha pauni 140,000.
Endapo watakamilisha mazungumzo yao na kupewa mkataba, basi Ozil atazidi kuchukua fedha nyingi kwenye klabu hiyo.
Wachezaji hao wamekuwa na mchango mkubwa katika klabu ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi, huku ya kwanza ikishikwa na Manchester City ila wanatofautiana kwa mabao.