Leonard Mangoha -Dar es salaam
MWENYEKITI wa Chama NCCR- Mageuzi, James Mbatia, ametangaza safu mpya ya viongozi wa juu itakayokiongoza chama hicho kwa miaka mitano.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbatia aliwataja viongozi waliochaguliwa na mkutano mkuu kuwa ni Katibu Mkuu, Elizaberth Mhagama, manaibu katibu wakuu Mussa Kombo Mussa (Zanzibar) na Rehema Kahangwa (Bara), huku makamu wenyeviti wakiwa ni Haji Ambari Hamis (Zanzibar) na Angelina Muthakiwa (Bara).
“Hii ndiyo safu ya viongozi wakuu sita ikiongozwa na mimi, uchaguzi ulikuwa huru na haki, tulianza Ijumaa tukakaa hadi usiku wa manane, tukamaliza jana usiku. Kwenye safu yetu ya uongozi tumejaribu kuzingatia usawa wa jinsia,” alisema Mbatia.
Katika hatua nyingine, Mbatia aliwataka wananchi kutoruhusu taifa ligawanyike kwa misingi ya udini, ukabila, sehemu ambayo mtu anayotokea, rangi wala jinsi gani na kwamba masuala ya watu kuringia vyama vyao ni mambo yasiyo ya msingi na yasiyo na tija kwa taifa.
“Ili kusisitiza hilo, ndiyo maana mtaona kwenye mkutano wetu mkuu hatukuweka bendera yoyote ya NCCR Mageuzi, tumesisitiza umoja wa kitaifa zaidi, ili kuhakikisha tunakuwa kielelezo japo kufanikiwa ni vigumu, lakini tumejitahidi,” alisema Mbatia.
Pia Mbatia ameiomba Serikali kukamilisha haraka kanuni mpya za uchaguzi na kuziweka wazi ili wadau wazipitie na kuzielewa kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofayika baadaye mwaka huu.