29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wawili CCM wawavaa kina Kinana

mwandishi wetu – dar es salaam

SIKU chache tangu Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, kuwavaa makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, wabunge wengine wawili wa chama hicho nao wameibuka wakiwapinga wastaafu hao.

Wiki iliyopita Kinana na Makamba waliandika barua kwa Baraza la Wazee wa CCM, wakitaka chama kichukue hatua dhidi ya mtu anayewachafua, huku akijipambanua kuwa mwanaharakati huru anayepambana na wanaomuhujumu Rais Dk. John Magufuli.

Kutokana na hilo, Bashe alisema waraka huo una malengo ya kugawa chama na kuwataka viongozi hao wastaafu wapambane na mtu huyo bila kuingiza chama kwenye vita yao.

Jana, Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, naye alisema yeye si shabiki wa mwanaharakati huyo, lakini Watanzania watafakari kwa kina taarifa ya wastaafu hao.

“Nilitarajia kwenye taarifa kwa umma ya wazee wetu Makamba na Kinana ningetegemea kupata majibu ya baadhi ya hoja ya anayewatuhumu.

“Hoja hizo ni je, yanayoyasemwa ni ya uongo? Kama yanayosemwa juu yao na makuwadi walioko nyuma ya pazia ni uongo, kwanini wasiende mahakamani kutafuta haki kwenye chombo cha sheria ya mahakama?

“Je, wazee hawa wanaweza kutuonesha iko wapi ndani na nje ya CCM kinga yao ya kikatiba ya kutokosolewa?

 “Je, viongozi hawa wastaafu walikosa njia sahihi ya kupeleka ujumbe wao kwa Baraza Ia Ushauri Ia chama kinyume na njia waliyotumia?

 “Je, wana uhalali gani wa kisiasa wa kutumia nembo ya CCM ilihali wao ni wastaafu kwenye nafasi walizowahi kuhudumu ndani ya chama?

“Je, mzee Makamba na Kinana wana uhalali gani wa kisiasa (moral authority) ya kukosoa CCM ya Dk. Magufuli  iliyorudi kwenye misingi iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kinyume na CCM yao waliyohudumu kwenye vipindi tofauti ambayo dhamira yake ilikuwa ni kuhudumia wachache ambao ni matajiri (mafisadi)?” alihoji Millya.

Akihojiwa na kipindi cha Tuongee Asubuhi cha Star Tv jana, Mbunge wa Geita Mjini, Joseph Msukuma, alisema waraka wa wastaafu hao umewafanya waamini wanazo njama kubwa.

“Ule waraka umetufanya tuamini kumbe yule (Cyprian) Musiba sio kichaa, ni mwanaharakati, anaeleza mpango wa kihuni unaofanywa na hawa wazee.

“Jana niliandika kwenye group la Bunge kuwa uvumilivu una mwisho, huwezi kumwita Rais mshamba na amechanganyikiwa.

“Huo waraka ni wa kijinga, hawa wazee wakiendelea tutawapiga na tutasema uozo wao maana kati ya hao wazee wapo waliokuwa wanaingiza makontena kwa wizi, wamwache Rais, na mimi namshauri Rais asiwasikilize,” alisema Msukuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles