32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu: Kesi zote ziwe na dhamana

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amependekeza kufanyika marekebisho ya sheria yatakayoruhusu watuhumiwa wa makosa yote yakiwamo ya mauaji na uhujumu uchumi kupewa dhamana ili kupunguza msongamano magereza.

Kauli hiyo imekuja siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli alipotembelea Gereza la Butimba jijini Mwanza na kukuta idadi kubwa ya wafungwa, na kusema baadhi wamebambikiwa kesi huku wengine wakiwa na kesi ndogondogo.

Hivi karibuni, pia Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alisema baada ya ziara aliyofanya magereza mbalimbali, amebaini uwepo wa msongamano mkubwa wa watu na kwamba wengi ni mahabusu.

 “Jambo ambalo mpaka sasa nimeliona ni ‘ratio’ (kiwango) ya watu waliopo magerezani ni kubwa kuliko uwezo wake, yaani kila palipo na mfungwa mmoja kuna mahabusu wanne.

“Sasa kwanza nitaanza kuhakikisha mahakama za mwanzo na wilaya zinajengwa, pia tutaangalia idadi ya watumishi,” alisema.

Pia Agosti mwaka jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliliambia Bunge kuwa magerezani kuna zaidi ya wafungwa 40,000 wakati uwezo wake ni  wafungwa 30,000.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP Rajabu Hamza, hivi karibuni alisema magereza ya Butimba, Kasungamile, Ukerewe, Magu na Ngudu yote kwa pamoja uwezo wake ni kupokea wahalifu 1,249, lakini sasa wapo 2,633 ikiwa ni ongezeko la wahalifu 1,384.

JAJI MKUU

Profesa Juma akizungumza jana wakati wa mahafali ya 60 ya mawakili wapya katika Shule ya Sheria, Dar es Salaam, alisema ikiwa mahakama itaachiwa haki ya kusimamia dhamana kwa kuifanya sheria isizuie dhamana kwa baadhi ya makosa kama ilivyo nchini Kenya, itasaidia kuondoa msongamano magerezani.

“Sisi mahakama tuna mapendekezo ya kutoa, kwanza tuwe kama Kenya, makosa yote yapewe dhamana, makosa yote mahakama iachiwe haki ya kusimamia dhamana, yaani sheria isifunge dhamana, hatutakuwa na hilo tatizo.

“Kenya hata kesi za mauaji mahakama inatoa dhamana, nadhani mnafuatilia na kuona inawezekana kabisa. Vilevile masharti ya dhamana inabidi tuyalegeze, kwa mfano sasa hivi wananchi wengi wana vitambulisho vya taifa, kwanini visitumike kama dhamana bila kumtaka mwananchi aoneshe mali?” alihoji Profesa Juma.

Alisema ikiwa jamii itazifuata changamoto hizo, itasaidia kupunguza tatizo hilo katika magereza mengi nchini.

Jambo jingine aliloshauri kufanyika ni kuhakikisha masuala ya kijamii, hususani yanayohusu mikataba, kushughulikiwa kwa kufuata makubaliano ya mikataba husika badala ya kuwakamata watu na kuwaweka mahabusu.

“Ni vizuri watu waliangalie, siku hizi kuna mtindo masuala ya kijamii kwa mfano mikataba au masuala yanayohusu ‘contractor’ (mhandisi) ameshindwa kukamilisha kazi yake, utasikia kamata weka ndani, hizo zote zinachangia.

“Tuache masuala ya jinai yaende kijinai na masuala yanayohusu masuala ya mikataba yaende kimkataba.

“Sasa mimi mchango wangu ni huo, kwamba tatizo siyo la mahakama peke yake, kwamba tatizo ni la ujumla zaidi, tupunguze adhabu ndefu, tupunguze adhabu ambazo hazina dhamana, tuwe wawazi zaidi kuwaruhusu watu wajidhamini wenyewe tutapunguza watu katika magereza yetu,” alisema Profesa Juma.

Aidha alisema kuwa sheria zetu zinaegemea zaidi kwenye adhabu kubwa, hasa kwa kesi zinazohusu mauaji, dawa za kulevya, uhujumu uchumi na ubakaji na vilevile upelelezi wake unachukua muda mrefu kukamilika.

Profesa Juma alisema kutokana na kuchelewa kukamilika kwa upelelezi, wanaopaswa kulaumiwa hasa ni wapelelezi siyo mahakama wala mtu mwingine.

“Upelelezi unachukua muda mrefu na sababu wanazotoa mahakamani kwanini upelelezi haujakamilika hazina mashiko, kwa sababu wao wana taratibu zao.

“Kuna tangazo moja ambalo lilitolewa na Mwendesha Mashtaka (DPP) mwaka 2012, kwamba kuna makosa ambayo usikamate mtu kama hujakamilisha upelelezi.

“Kwa bahati mbaya hilo halifuatwi, watu wanakamatwa ndiyo upelelezi unakwenda kufanyika, kwa hiyo hiyo imechangia.

“Vilevile wananchi inabidi tubadilike, tumekuwa tukipenda adhabu kali zaidi badala ya kutoa adhabu mbadala’

“Ukisikiliza mahojiano bungeni, kila mtu anataka adhabu kali miaka 30 miaka 15, hizo zote zinachangia magereza kujaa,” alisema Profesa Juma.

Kuhusu sheria inayoruhusu mahakimu kufuta kesi ambazo upelelezi wake umeshindwa kukamilika kwa muda mrefu, alisema licha ya sheria kueleza hivyo, lakini baada ya mtuhumiwa kuachiwa hutakiwa kukamatwa tena jambo ambalo ni sawa na bure.

Alisema ili sheria hiyo ifanye kazi, ni vema kukubali sheria itamke wazi kwamba ukifika muda fulani upelelezi haujakamilika kesi ifutwe na kwamba hilo likifanyika mahakama itatekeleza.

Kuhusu mahabusu na wafungwa kutolewa gerezani, alisema mwenye uwezo wa kufanya hivyo ni mahakama pekee na si mtu mwingine yeyote.

“Mtu yeyote asikwambie ana uwezo wa kumtoa mtu gerezani bila amri ya mahakama, hilo ni moja, suala lingine huu ni wakati mzuri kuzungumzia adhabu zinazotolewa. Vilevile ni wakati mzuri kuzungumzia upelelezi unaochelewa,” alisema.

Profesa Juma alisema mahakama inaweza kutunza kumbukumbu vizuri na kwamba hata Gereza la Butimba lilitembelewa na mahakimu Julai 4 kabla ya ziara ya Rais na mambo ambayo yameonekana wakati wa ziara ya Rais, na wao waliyaona na kusisitiza kuwa hayo ni matokeo ya upungufu katika sheria za nchi.

Kuhusu malalamiko mbalimbali ambayo yamekuwa yalitolewa na wananchi kuwa baadhi ya watendaji wa mahakama wamekuwa wajihusisha na rushwa hali inayosababisha kutotenda haki, alisema wao wako wazi na hawaogopi kukubali kuwa rushwa ni tatizo.

“Ukifika mahakamani utakuta bango linakueleza wazi kwamba rushwa haikubaliki.

“Rushwa usipoizungumza haitatoka, kwa sababu rushwa huwa inajificha, sasa sisi tumejitokeza kwamba rushwa tunaiongelea na ukiangalia watumishi wengi hapa wamevaa mabango maana yake nini, kwamba anayekuomba rushwa mtaje.

“Usizungumzie rushwa kiujumla na kama mnavyofahamu tunachukua hatua, anayepatikana na kosa la rushwa hatumrudishi tena kwenye kazi.

“Tunatumia falsafa ya Mwalimu Nyerere, aliyesema kwamba kazi ya uhakimu na ya ujaji ni kazi takatifu, hutakiwi hata kushukiwa kwamba unajihusisha na rushwa. Kwa hiyo tuko wazi kabisa kwenye suala la rushwa.

“Kama kuna suala la rushwa msione aibu kuja kutwambia au kwenda Takukuru, na kwa bahati nzuri siku hizi teknolojia imekuwa ni nzuri zaidi, mtu anayekuomba rushwa unaweza kumrekodi, unaweza kumpiga picha na tumeweza kutumia baadhi ya utaalamu huo kuwanasa waliokuwa wakihusika na rushwa,” alisema Profesa Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles