Tunu Nassor – Dar es Salaam
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imevitaka vyuo vikuu nchini kuweka bajeti ya kutosha ya wanafunzi kufanya tafiti ili waweze kufanya kazi za ubunifu kidigitali.
Akizungumza kwenye maonyesho ya 14 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia jijini Dar es Salaam, leo jumatano Julai 17, Kaimu Mkurugenzi wa Maarifa, Emmanuel Nnko, amesema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia dunia nzima imekuwa ikifanya shughuli zake kidigitali hivyo ni vyema kubadilisha mifumo ya ufanyaji tafiti kuendana nayo.
Amesema ili vyuo vikuu kuweza kufanya tafiti kidigitali ni vyema vikaweka bajeti ya kutosha kuwapatia maarifa ambayo yatawawezesha kufanya kazi kidigitali.
Akizungumzia majukumu ya COSTECH amesema ina jukumu la kuhamasisha, kuratibu na kuendeleza tafiti na Maendeleo ya Teknolojia hapa nchini.
Kwa upande wake, Dk.Magreth Mushi kutoka Mtandao wa Taasisi za Elimu na Utafiti Tanzania (Ternet), ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano na COSTECH amesema hali ya Sasa kidunia vyuo vinapaswa kuendesha shughuli zake kidigitali.
“Mtandao wa taasisi za elimu na Utafiti Tanzania tuna jukumu la kuunganisha vyuo na sasa tuna jumla ya vyuo zaidi ya 49 ambavyo vipo katika mtandao na kati ya hivyo 30 vipo kwenye mradi wa elimu ya juu na Utafiti,” amesema Magreth.