Beatrice Mosses – Manyara
Mkuu wa Taasisis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Manyara, Fidelis Kalungura, ametoa tahadhari kwa watu wanaojifanya ni maofisa wa taasisi hiyo ambao huwapigia watu simu na kuwatisha kwa lengo la kujinufaisha au kuchafua kazi inayofanywa na taasisi hiyo.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo ameomba ushirikiano wa hali ya juu kwa waandishi pamoja na wananchi kusaidia kupambana na tatizo hilo.
“Tunawaomba wananchi wote kuendelea kutupa ushirikiano na kuunga mkono mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa pia tunawaomba wasiwe watazamaji bali washiriki kwa vitendo katika vita hii dhidi ya rushwa kwani hilo sio jukumu la Takukuru peke yake bali ni la kila mmoja wetu,” amesema.
“Takukuru hatuiti mtu tukakutane mtaani, bali tunamuita mtu aje ofisini na kwa taratibu zinazokubalika kwa hiyo pale linapojitokeza jambo la namna hiyo tupeni ushirikano, tupeni taarifa kusudi tuweze kuchukua hatua za haraka dhidi ya watu wa namna hiyo wanaochafua kazi zinazoendelea lakini pia wanaotuchafua”, amesema.