25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Masauni aeleza kusikitishwa na aliyoona kwenye magereza

BENJAMIN MASESE-MWANZA

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad  Masauni, amesikitishwa jinsi mahabusu na wafungwa walivyojaa katika magereza akidai wengine wapo humo kutokana na kuonewa.

Kutokana na hali hiyo aliagiza wakuu wa magereza nchini, makamanda wa polisi, kamati za kuharakisha kesi na watumishi wengine wa wizara hiyo, kuanza kuwasikiliza mahabusu na wafungwa katika magereza yote nchini na kupitia upya sababu zilizowafanya kuwekwa magerezani.

Agizo hilo alilitoa jana jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya majumuisho ya ziara yake katika mikoa ya Tabora, Geita na Mwanza.

Katika ziara hiyo, alitembelea magereza mbalimbali likiwamo la Butimba na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu ambapo alisema ameshuhudia na kuelezwa mambo ya ajabu.

Masauni alisema  akiwa Mkoa wa Tabora alikutana na mwanamke aliye na mtoto na amewekwa mahabusu  miezi mitano bila kupelekwa mahakamani  jambo ambali alisema si la kiungwana.

“Suala la magereza kujaa hili ni tatizo sugu hapa nchini lakini nimepata picha fulani baada ya kutembelea magereza ya Tabora, Geita na leo (jana) nipo Mwanza katika gereza kuu la Butimba, niwaambie kabisa bila kificho huu msongamano tunaosema kila siku  kwa asilimia kubwa sisi viongozi  hasa wakuu wa magereza, makamanda wa polisi na zile kamati za kuharakisha kesi, hamfanyi kazi zenu.

“Hii tabia ya kusubiria mpaka viongozi wa kitaifa tuje mikoani kuwaelekeza cha kufanya katika maeneo mnayoongoza naomba mbadilike, nasema muda wenu wa kushikilia nafasi zeni upo katika matazamio kama hamtawajibika kwa kujiwekea malengo.

“Kuanzia sasa nataka kusikia mmeanza vikao vya kuwasikiliza mahabusu na wafungwa kwa kila mmoja kilichosababisha akaletwa humo, yapo mambo mengine yanayohitaji kuyatatua au kuwasaidia wale watu.

“Wapo wanaoletwa humo kwa kuonewa na wengine wamekosa msaada wa kuwaelekeza, kaeni nao mjue namna ya kuwasaidia, hili ni agizo la kitaifa si la hapa kanda ya ziwa vinginevyo vyeo vyenu vitawatoka,”alisema.

Hata hivyo Masauni alimtaka Mkuu wa  Gereza  la Butimba, Hamza  Rajabu kumweleza anavyotekeleza sera ya Serikali ya viwanda ambapo alisema ndani ya gereza hilo kuna kiwanda cha ushonaji nguo na wamekuwa wakipata kazi mbalimbali kutoka wa mashirika ya umma na binafsi.

Licha ya kupewa majibu hayo, Masauni alisema alichogundua uongozi wa gereza hilio bado hauna mpango mkakati wa kuliwezesha gereza hilo kujitegemea kwa chakula licha ya uwepo na hekari 479 za kulima mazao mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mwanza.

Awali, Mkuu wa Gereza la Butimba, Rajabu alimweleza Masauni kuwa gereza hilo limezidiwa na watu kwani uwezo wake ni kuchuchua wafungwa 934 lakini waliopo sasa ni  1,888 na magereza yote ndani ya mkoa huo yana uwezo wa kuchukua  watu  1,249 lakini waliopo ni 2,633.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles