BENJAMIN MASESE-MWANZA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuwa imebaini utapeli na ukiukaji mkubwa unaofanywa na mawakala kutoka kampuni mbalimbali za mawasiliano nchini wakati wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole (biometric) unaoendelea.
Kutokana na hali hiyo, TCRA imefanya operesheni ya kushtukiza katika Jiji la Mwanza na kuwakamata mawakala mitaani ambao wanadaiwa kuhusika na utapeli kwa kusajili laini zinazojuliokana kwa jila la ‘Take away’ na kuwafikisha katika vituo vya polisi kwa hatua za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, alisema hatua hiyo imetokana na kupata malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kutapeliwa fedha na mawakala hao sambamba na kusajili laini mbili na kuwauzia watu wengine ambao hufanyia uhalifu ikiwamo utapeli.
Alisema kabla ya kufanya operesheni hiyo walijiridhisha kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa kwao na kulazimika kufanya msako nchi nzima kuanzia jana na kwa Mkoa wa Mwanza walifanikiwa kuwakamata mawakala zaidi ya 10.
“Tunapozungumza hapa zoezi la kuwakamata linaendelea mitaani, tayari mawakala zaidi ya 10 tumewatia nguvuni kwa kushirikiana na polisi, kama TCRA tumechukua hatua zaidi kwa kuwaandikia barua kampuni zote na kuwapa masharti na vigezo vinavyotakiwa kwa mawakala hao.
“Kwanza ni marufuku kwa mtu yeyote kuuza, kusambaza au kusajili laini za simu bila kuwa na uthibitisho wa kuidhinishwa na mtoa huduma za mawasiliano, pili yeyote anayejihusisha na uuzaji, kusambaza au kusajili laini za simu anatakiwa kuwa na ofisi ya kutolea huduma ya usajili na si kutembea barabarani,” alisema Mihayo.