Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Serikali imeanza uchunguzi wa chanzo cha ajali iliyoua watu saba wakiwamo wafanyakazi watano wa Azam Media ambapo tayari dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo amekamatawa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni, amesema hayo leo Jumanne Julai 9, wakati miili ya wafanyakazi hao ikiagwa katika Ofisi za Azam, Tabata jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea jana Julai 8, kati ya Shelui na Igunga baada ya gari aina ya Toyota Coaster kugongana uso kwa uso na lori.
“Nichukue fursa hii kuwajulisha kuwa uchunguzi wa ajali hiyo umeshaanza na unaendelea vizuri na tumeshamkamata dereva wa lori liligonga gari walilokuwamo wafanyakazi wa Azam, tunafanya uchunguzi tukishirikisha taarifa za mashuhuda wa ajali hiyo,” amesema Masauni.
Aidha, Masauni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani Tanzania, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.