Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Maelfu ya watu wakiongozwa na viongozi na wanasiasa wamejitokeza leo jumanne Julai 9, kwa ajili ya kuaga miili ya wafanyakazi watano wa Azam Media waliofariki katika ajali iliyotokea jana kati ya Shelui na Igunga.
Ajali hiyo ilitokea jana Julai 8, baada ya gari aina ya Toyota Coaster kugongana uso kwa uso na lori amabpo pia ilisababisha vifo vya dereva wa Coaster na utingo wake.
Ibada ya mazishi na shughuli za kuaga miili hiyo zinafanyika katika viwanja vya studio za Azam TV zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi na wanasiasa waliojitokeza kuaga ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, January Makamba, Mbunge wa Ilala, Mussa Assan Zungu (CCM), na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema), Freeman Mbowe.
Walikuwepo viongozi wa kimichezo akiwamo Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Crescetius Magori na Msemaji wa Klabu hiyo, Haji Manara, Msemaji wa Yanga, na Afisa Habari wa Klabu ya Yanga, Dismas Ten.
Aidha wafanyakazi wa Azam Media waliofariki katika ajali hiyo ni Charles Wandwi, Florence Ndibalema, Said  Hassan,  Salim Mhando na Silvanus Kasongo.