CHRISTIAN BWAYA
KILA mzazi hutamani mwanawe afanye vizuri katika maeneo yote ya kimaisha. Tunatamani wanetu wawe na mwenendo safi na tabia njema; wafanye vizuri shuleni; wawe na nidhamu ya maisha ili hatimaye waweze kufanikiwa maishani.
Kwa sababu hiyo, hapa na pale wazazi tunawajibika kuwaelekeza kufuata njia tunayojua wanapaswa kwenda; tunawakemea kwa kuwaadhibu tabia zisizofaa kila zinapojitokeza; lengo ni kuhakikisha wanakuwa watu wanaojitambua wafikie ndoto zao.
Lakini wakati mwingine, lugha tunayoitumia kwa nia njema kabisa inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Kwa maana nyingine, shauri ya lugha tunayoitumia, bila kutarajia, kile tulicholenga mtoto akielewe kinaeleweka vingine kinyume na matarajio yetu.
Tuchukulie mwanao amefanya vibaya darasani, kwa kutamani afanye vizuri unamwambia, ‘Hebu jitahidi mwanangu. Alama hizi unazopata hazifai. Mimi sijawahi kupata alama hizi. Nilipokuwa na umri kama wako, nilikuwa na bidii kwenye masomo. Kwa sababu ya kufanya bidii, siku zote nilishika nafasi kati ya nambari moja na tatu darasani!’
Lengo ni jema kabisa. UnaÂchofikiri hapo ni kuwa mwanao akisikia simulizi la mafanikio yako, atahamasika na kuanza kujitahidi. Unafikiri uwezo wako ulipokuwa katika umri wake unaweza kumtia hamasa kijana. Inawezekana ikawa hivyo. Lakini mara nyingi mambo huwa kinyume.
Unapomwambia kijana namna ulivyokuwa ukifanya vizuri, unaweza kuibua hisia mchanganyiko. Kijana wako anaweza kusikia ujumbe toÂfauti na huo. Kichwa chake kinaweza kuchakata taarifa tofauti kabisa. Ujumbe huo huo ukasikika, ‘Mimi baba yako nilikuwa mtu mwenye akÂili. Nilipokuwa na umri wako, sikuwa mjinga kama wewe. Nilijituma sio kama wewe unayeendekeza uvivu.’
Tafsiri hiyo inafanya nafsi ya mtoto ijisikie kudhalilika. Na kwa sababu hakuna mtu hufurahia kuÂjisikia dhalili, mtoto atakabiliana na kauli hiyo kwa kukupinga. Pamoja na nia njema uliyonayo bado mawazo ya mtoto yanaweza kuwa hasi; ‘Baba anajiona kichwa sana kuliko mimi. Hapa ameniita kunitambia alivyokuÂwa anaongoza darasani. Shule siku hizi ngumu. Mazingira yamebadiÂlika.’
Kijana mwenye mawazo kama haya hawezi kubadilika hata kama ungeongea mpaka kesho. Ukitaka mtoto akuelewe kirahisi, zingatia ukweli kuwa kwa hulka zetu, huwa tunavutiwa na wale wanaofanana nasi; wanaoishi maisha kama yetu; wenye changamoto kama zetu na wale wanaoonesha kuelewa maisha yetu.
Nasaha na ushauri mwingi mzuri hukosa kibali kwa watoto kwa sababu sisi wazazi wakati mwingine tunatumia nguvu nyingi kujitofautiÂsha na wanetu. Mfano, mzazi anaonÂgea na vijana wenye changamoto za uhusiano ujanani.
Pengine kwa kufikiri anaweza kuwahamasisha, anatumia muda mwingi kusimulia namna yeye alivyokuwa na ‘ujana mtakatifu.’ Vijana hawa ambao tayari hawana huo utakatifu, wanajisikia dhalili. Hawatamsikiliza kwa dhati.
Fikra zao zitakata mawasiliano na kuanza kuhoji ukweli wa yanayÂosemwa; tofauti ya mazingira ya wakati huo na haya waliyonayo wao na kwa kweli uwezekano wa wao kupokea ujumbe huo ni mdogo.
Hoja yangu ni kwamba mapunÂgufu yako mzazi, makosa na udhaifu wako ukivisema vizuri kwa lugha ya unyenyekevu, vinaweza kuwa na nguvu ya kumbadilisha mwanao kuliko masimulizi ya mafanikio.
Kwa wazazi, kama kweli unataka kijana wako ahamasike kuchukua hatua za kubadilisha tabia yake, huna sababu ya kumsimulia namna ulivyokuwa bora kuliko yeye. Mfanye ajione kwenye maisha yako. Atahamasika kubadilika.