23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Vyakula vya moto ndani ya plastiki huvuruga homoni mwilini

AVELINE KITOMARY

MATUMIZI ya mifuko ya plastiki kwa sasa yamekuwa yakipigwa vita duniani kote, huku wadau mbalimbali wa mazingira na Umoja wa Mataifa wakishawishi mataifa mbalimbali kuachana na matumizi ya mifuko huyo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa [UN] inaonyesha nchi 60 duniani tayari wameshapiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, huku tukishuhudia nchi zingine zikiendelea kutanganza marufuku ya mifuko hiyo.

Vita dhidi ya mifuko ya plastiki inatokana na uharibifu wa wazi wa mifuko hiyo hasa kwa mazingira na mifugo.

Kwa Afrika Mashariki, nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda na Tanzania tayari wameshapiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo na hadi sasa juhudi hizo zinaone­kana kufanikiwa kwani mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutekeleza marufuku hiyo.

MADHARA KWA AFYA

Mifuko ya plastiki inamadhara katika mwili wa binadamu, kwani kemikali zilizopo katika mi­fuko hiyo zinauwezo wa kuvuruga homoni zilizopo mwilini.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Kheri Tungaraza, anasema matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kuwekea vyakula au vinywaji hasa vile vyenye joto la juu husababisha madhara mwilini.

“Plastiki nyingi huwa zinaten­genezwa na Hydrocarbon, kemikali hizi zikipata joto zinaweza kuy­eyuka zikaenda kwenye chakula au kinywaji na hivyo mlaji kupata madhara kiafya.

“Moja ambayo inaushahidi wa kutosha ni zile kemikali kwenda kwenye mwili na kuvuruga wingi au kawaida ya homoni, hizo homo­ni zikivurugwa zinaweza kuleta matatizo ya uzazi.

“Kuna saratani zinazochochewa na homoni kama ya matiti huto­kana na homomoni ya Oestrogen (homoni za kike) kuathirika au saratani ya tezi dume inachochewa na Testrosterone (homoni za ki­ume),” anaeleza Dk. Tungaraza.

Anaongeza: “Kemikali zina­zotoka kwenye plastiki zinaweza kuongeza au kupunguza kiwango cha homoni hivyo kuleta mvu­rugiko utakaobadilisha mzunguko wa hedhi.

Dk. Tungaraza anabainisha kuwa watu wanaotumia zaidi bidhaa za plastiki ambazo hazina ubora, wako katika hatari kubwa ya kupata mvurugiko wa homoni.

Anasema kwa sasa hakuna tak­wimu sahihi za kujua kiwango cha madhara ya plastiki mwilini.

“Hamna tafiti zinazoonesha moja kwa moja kuwa saratani kad­haa zinasababishwa na matumizi ya plastiki.

“Bado Shirika la Afya Duni­ani (WHO) hawajatenga plastiki kama kisababishi cha saratani na hawawezi kufanya hivyo kutokana na kukosa ushahidi wa kutosha,” anasisitiza Dk. Tungaraza.

Anasema inakuwa ngumu kwa­sababu kuna vitu vingi vinavyo­sababisha saratani kama kutumia plastiki, kuvuta sigara, unywaji wa pombe na mazingira machafu.

“Ni vigumu moja kwa moja kusema kisababishi ni plastiki kwani vipo vingi ila tunahofia kuwa zile kemikali zinaingia mwilini na kuleta madhara tofauti tofauti.

“Kutokuwa na ushahidi wa kutosha haimaanishi kuwa haina madhara, kwa sababu tunaona plas­tiki zinatengenezwa na kemikali viwandani,” anasema.

UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Mifuko ya plastiki husababisha uharibifu mkubwa utokanao na kutupwa hovyo na kuzagaa katika mazingira.

Plastiki zikichomwa moto moshi wake unaathari kwa afya ya binadamu kutokana na kemikali iliyopo katika plastiki. Wananchi wengi wamekuwa wakiitumia mifuko laini ya plastiki kuwashia moto kwenye majiko ya mkaa.

Mifuko hiyo haiwezi kuoza kwa haraka katika ardhi inakadiriwa ku­weza kudumu hadi zaidi ya miaka 500 hivyo ikitupwa hovyo inazagaa na kuongezeka katika ardhi kuleta kero kwa binadamu na viumbe wengine.

Katika shughuli za kilimo ni vigumu kwa mizizi ya mimea kupenya plastiki zilizopo ardhini na kuukuta udongo ili kujipatia maji na madini kwaajili ya ukuaji wa mimea. Jambo hili huzuia ustawi wa mimea na kupelekea uhaba wa chakula na hewa safi kutoka kwa mimea.

Kutokana na mifuko hiyo, kuwa ya bei rahisi mara nyingi matumizi yake huwa ni mara moja tu kwa kubebea bidhaa na kisha hutupwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Maka­mu wa Rais (Muungano na Mazin­gira), January Makamba, anasema tangu mwaka 2003 serikali ilikuwa na mpango wa kupunguza mifuko ya plastiki.

“Miaka 15 iliyopita serikali ilikuwa ikipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kupandi­sha kodi, sasa hivi agenda kubwa ya mazingira ni kupiga vita bidhaa hizi,” anasema Makamba.

Anasema Dunia nzima sasa inaelekea kupiga marufuku ku­tokana na taka za plastiki kuzidi baharini kwani taka hizo haziozi wala kuyeyuka.

“Utafiti unaonesha asilimia 90 ya taka za plastiki zimeishia baha­rini na inasemekana kadri miaka inavyoenda taka hizo itakuwa nyingi kuliko samaki.

Anaongeza: “Taka hizo zina madhara makubwa kwa mazingira na bahari,

mifereji kuzibika chanzo chake ni utupwaji hovyo wa mifuko ya pastiki.

VIFO VYA MIFUGO

Wakati mwingine wanyama ķama ng’ombe, kondoo na mbuzi wanapenda kula mifuko ya plastiki kutokana na kuwekwa chakula chenye chumvi na wao hupenda vyakula vyenye ladha ya chumvi.

Wanyama wakimeza mifuko hiyo haiwezi kumeng’enywa hivyo hubaki tumboni na kuendelea kukusanyika zaidi tumboni, hatimaye huweza kuziba njia ya chakula na kusababisha chakula kidogo kuruhusiwa kupita katika mfumo wa umeng’enyaji.

Madhara yake yanaweza kuonekana baada ya muda fulani, wanyama wenye mifuko ya plastiki tumboni mara nyingi hupunguza kiwango cha kula na kuanza ku­konda hata akipewa dawa hawezi kupona, matokeo yake hufa.

Wanyama waliokufa wakika­pasuliwa hukutwa na mifuko ya plastiki ndani ya matumbo yao.

Kwa wanyama wadogo kama kuku, bata na aina nyingine za ndege, wanaweza kujiviringishia kichwani, hii husababisha kukosa hewa na wasipopata msaada wa haraka hufa.

Hivyo basi, kupigwa marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ni njia nzuri ya kuepusha vifo vya wanyama.

WADAU MAZINGIRA

Mkurugenzi wa Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), John Chikomo, aliliambia MTANZANIA kuwa tamko lililotolewa na serikali la ukatazwaji wa mifuko ya plastiki ni moja ya mafanikio kwao.

“Sisi wadau wa uhamashishaji wa utunzaji mazingira tamko hili tumelipenda, tumelipokea kwa mikono miwili hivyo kutakuwa bega kwa bega na serikali kupeleka ujumbe kwa jamii.

“Tutaendelea kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa ku­tunza mazingira kwaajili ya kizazi kijacho,” anasema Chikomo.

SHERIA IMESAIDIA

Sheria zilizowekwa zimesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kua­cha mara moja matumizi ya mifuko hiyo.

Kanuni namba 8 ya sheria ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plas­tiki ya mwaka 2019 inaeleza juu ya makosa yanayotokana na uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, kuhifadhi, kuagiza na kuingiza.

Adhabu iliyoainishwa kwa wan­aohifadhi na kusambaza faini ni Sh milioni tano hadi milioni 50 pamoja na kifungo cha miaka miwili jela. Kwa upande wa wauzaji watatozwa faini isiyopungua Sh 100,000 hadi 500,000 pamoja na kifungo cha miezi mitatu jela huku upande wa mtumiaji faini Sh 30,000 na jela siku saba.

Juhudi za serikali kukataza matumizi ya mifuko hiyo ni nzuri kutokana na madhara yanayosaba­bisha ikiwamo vifo vya mifugo, uharibifu wa mazingira na mad­hara katika afya ya binadamu hata viumbe hai wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles