Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
KAULI iliyotolewa na Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua akiwataka Watanzania na Waganda wanaofanya biashara nchini humo kuondoka ndani ya saa 24 vinginevyo watawatoa kwa nguvu, imeibua jambo bungeni.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alitoa kauli ya Serikali akitaka Watanzania kuwa watulivu.
Hata hivyo, mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki, akifahamika zaidi kwa jina la Jaguar, alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kudai kauli aliyoitoa iliwalenga Wachina ambao wamevamia masoko ya Wakenya kuendesha biashara zinazoweza kufanywa na Wakenya.
Akitoa kauli ya Serikali jana, Majaliwa alisema Serikali imechukua hatua dhidi ya kauli hiyo ikiwa ni pamoja na kumwita Balozi wa Kenya nchini kufahamu msimamo wa kauli hiyo, ambaye ameeleza huo sio msimamo wa nchi yake.
“Jambo hili tumeanza kulisikia jana (juzi) usiku. Hatua tuliyoanza nayo ni kumtambua mzungumzaji ana nafasi gani. Nchi ya Kenya ni wenzetu, rafiki na nchi jirani hata viongozi wetu wakuu wanazungumza lugha moja.
“Tumemwita Balozi wa Kenya nchini na pia tumezungumza na Balozi wa Tanzania nchini Kenya. Balozi wa Kenya amekanusha kuwa kauli ile si kauli ya Serikali na wala sio msimamo wa Kenya, wametusihi Watanzania tuwe watulivu, kauli hiyo ni ya mtu mmoja,” alisema Majaliwa.
Aidha, alisema wakati kauli ya mbunge huyo ikitolewa, vikao vya Bunge la Afrika Mashariki vinaendelea Arusha ambako mawaziri wamelaani kauli hiyo.
Waziri Mkuu alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya Spika Job Ndugai kuiagiza Serikali kuja na majibu ya kuwahakikishia usalama Watanzania wanaoishi nchini Kenya.
Ndugai alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa, kutaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu usalama wa raia wa Tanzania waishio Kenya.
Akijibu mwongozo huo, Spika aliiagiza Serikali kuja na majibu haraka kutokana na jambo hilo kuwa muhimu kwa usalama wa Watanzania.
Jioni mara baada ya wabunge kupiga kura, Spika aliomba ushauri kwa wabunge kuhusu jambo hilo.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema jambo hilo ni kubwa na Serikali inatakiwa kulitolea jibu.
“Hili jambo ni kubwa na zito, sio la kupuuza, alichokizungumza Mbunge wa Kenya nilikiona jana usiku na niliwauliza viongozi wengi wa Kenya walikana, sio kauli nzuri, sisi kama Watanzania kama tumetajwa tunahitaji majibu, sidhani kama tuna sababu ya kupuuza.
“Nashauri Bunge litoe kauli ya kulaani na itambue hatuna ugomvi na Kenya, lakini tuitake Serikali ya Kenya kudhibiti hili kwani linaweza kuchafua hali yetu,” alisema.
Mbunge wa Buchosa, Dk. Charles Tizeba alisema mambo hayo yametokea katika nchi nyingi Afrika, hivyo Serikali haitakiwi kulipuuza.
“Yule mbunge unaweza ukamdharau, mambo haya yameishatokea hapa Afrika kwa uchochezi mdogo mdogo kama huu hapa, hatuichukii Jamhuri ya Kenya, lakini Serikali ya Kenya inayo jukumu la kukana hiyo kauli. Kama nchi iseme sisi hatuko nae huyo,” alisema.
Mbunge wa Bulyanhulu, John Kadutu, alitaka Wizara ya Mambo ya Nje kupewa kazi ya kulishughulikia jambo hilo.
“Mimi ushauri wangu hapa tunayo wizara, jambo hili sio la kupuuza, Bunge liiagize wizara wawasiliane na wizara. Kama tunatajwa ni Watanzania na aliyetaja ni mbunge tusikae kimya,” alisema.
Mbunge wa Mtera, David Lusinde alishangaa wabunge kujadili mtu mmoja ambapo amedai kwamba huo ni woga.
“Mbunge mmoja tunatumia kumjadili kama nchi, nitatoa amri tuwapige warudi kwao Kenya, huu huu ni woga,” alisema hali ambayo ilimlazimu kusimama Waziri Mkuu kulitolea ufafanuzi.