28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ataka mradi wa Dege ufanyiwe tathmini

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameagiza kufanywa tathmini ya mradi wa majengo ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika eneo la Dege Beach Kigamboni, Dar es Salaam ili yaweze kupangiwa matumizi mapya. 

Mradi huo wa nyumba 7,460unajengwa kwa ubia kati ya NSSF na Kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (AHEL).

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa ghala na mitambo ya gesi ya Kampuni ya Taifa Gas, Rais Magufuli aliagiza kutolewa kwa haraka mawazo ya matumizi mapya ya majengo hayo kwani yamekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.

“Yale majengo ya NSSF yamekaa kwa muda mrefu na ni mradi bomu, wa ovyo na wa kifisadi. Tumeshawaeleza haya NSSF pamoja na bodi washughulikie, watoe mawazo yao na nyie wananchi mtoe mawazo yenu tuone jinsi gani haya majengo tunaweza kuyatumia katika njia iliyo sahihi.

“‘Investment’ kubwa kama hiyo imekaa na wala hatutoi majibu. Kama ni kuyatoa yawe mabweni ya chuo au nyumba za wafanyakazi tusubiri uchambuzi utakaofanywa,” alisema Rais Magufuli.

Novemba mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alitembelea mradi huo na kusikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaoendelea katika eneo hilo na kuagiza ulinzi uimarishwe.

Mkataba kati ya NSSF na AHEL ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni hodhi ya ‘Hifadhi Builders’ ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45. 

Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa katika mradi na asilimia 35 kampuni hiyo ingetakiwa kuweka fedha taslimu.

Mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu Sh trilioni 1.5.

Hadi kufikia Juni mwaka jana, NSSF walishailipa Kampuni ya Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 kama mchango wake katika ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na Sh bilioni 305.8 wakati Kampuni ya Azimio ilitoa Dola 5,500,000 sawa na Sh bilioni 12.6 tu.

Awali kashfa ya mradi huo iliibuliwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/2014 na mwaka juzi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilibaini madudu katika utekelezaji wa mradi huo na kutoa mapendekezo kwa Bunge kwa hatua zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles