27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa Taifa Gas wamfurahisha JPM

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameeleza kufurahishwa na uwekezaji wa Kampuni ya usambazaji gesi za majumbani, Taifa Gas, ambao umewezesha kuongeza uwezo wa kuhifadhi nishati hiyo kutoka tani 1,650 mwaka 2016 hadi 1,750.

Uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 150, umeifanya Taifa Gas kuwa kampuni ya kwanza Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuwa na ghala na mitambo inayoweza kuhifadhi kiasi hicho cha gesi.

Kampuni hiyo ambayo zamani ilijulikana kama Mihan Gas, pia inapanga kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 500 katika sekta hiyo ya gesi ndani ya miaka mitano ijayo.

Rais Magufuli akizungumza jana wakati akizindua ghala na mitambo ya Taifa Gas, alieleza kufurahishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Rostam Aziz, ambaye ni mwenyekiti wa bodi wa kampuni hiyo na kumtaka kuleta wawekezaji wengine hata 20 nchini wa aina yake na Serikali itawaunga mkono.

 “Miongoni mwa kampuni za gesi zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi hapa nchini ni Taifa Gas iliyokuwa inaitwa Mihan Gas, kampuni hii kama mlivyosikia imewekeza Sh bilioni 150 ikihusisha ujenzi wa maghala na mitambo ya kuhifadhi kwenye mikoa 20.

“Na mojawapo ni hili ghala kubwa nililolizindua leo (jana), limeifanya Kampuni ya Taifa Gas kuongeza uwezo wa nchi yetu kuhifadhi gesi, pia kampuni hii imeongeza uwezo wa nchi yetu kuongeza gesi ya mitungi kutoka tani 8,050 mwaka 2016 hadi kufikia tani 15,600 hivi sasa.

“Nimefurahi kumwona mmiliki wa kampuni hii ni Mtanzania, kwa utekelezaji huu mkubwa mmenipa moyo kwamba Watanzania wanaweza hasa tunapoamua.

“Hivyo Rostam ninakupongeza kwa uwekezaji huu na kuwezesha ajira za hapa nchini kufikia 260, lakini zingine kutokana na gesi hii kufikia hadi 3,000. 

“Pia nimesikia mmelipia kodi na tozo mbalimbali Sh bilioni moja kwa mwaka, ni matumaini yangu haya malipo yatakuwa yanaongezeka kadiri gesi itakavyokuwa inaongezeka.

“Vilevile kama mlivyosikia sio gesi yote wanayoagiza inatumika hapa nchini, bali inatumika hadi nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Zambia, hii maana yake ni kwamba nchi yetu inapata fedha za kigeni,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa Rostam kwa kufanya uwekezaji kwa vitendo.

“Nakushukuru Rostam, nimefurahi sana na hiki ndicho ambacho nataka mimi, huwa sitaki wawekezaji wa maneno maneno tu, umeonyesha mfano, hii imenipa nguvu sana.

“Tafuta wawekezaji wengi hata 10 au 20 wenye moyo wa namna hii wa kuwekeza, tuje tuwape ‘support’, tunahitaji wawekezaji wa kweli waje, wasisikilize maneno ya wale ambao hawatutakii mema.

“Tukiwa na wawekezaji wa namna hii tutawasaidia na wanapowekeza tunataka wananchi nao wapate, ndio maana ya ‘win win situation’, naendelea kuwashukuru wawekezaji wa aina hii ambao watakuja kwa moyo wa namna hiyo.

“Pia Rostam umeniambia kuhusu kiwanda cha ngozi cha Morogoro ndani ya miezi mitatu, ahadi ni deni, nitakuja, nitahakikisha kukifungua kwa sababu sisi tuna mifugo mingi na Tanzania sisi wa pili au tatu Afrika, lakini hatuna kiwanda cha ngozi wakati tuna ng’ombe zaidi ya milioni 30, lakini ngozi tunaagiza nje ile ni ‘poor planning’,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, alisema kama kuna mwekezaji ambaye anaweza kuja nchini kuwekeza anakaribishwa.

“Akija aje awekeze kwenye ngozi na afanye mpaka kwenye ‘final product’, hapo tutavaa nguo, viatu vizuri kutokana na ngozi na wanyama wetu, kwa hiyo ‘opportunity’ ziko nyingi,” alisema.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wamiliki hao wa Taifa Gas pamoja na kampuni nyingine ambazo zinajishughulisha na biashara hiyo ya gesi na mitungi.

“Kuhusu mkurugenzi kueleza changamoto mliyonayo ya eneo, ni matumaini yangu kwamba mamlaka husika imesikia kwa sababu Tanzania hatujawahi kupungukiwa na ardhi. 

“Miradi hii huwa inanufaisha wananchi, hivyo kama utaendelea na wananchi watakuuzia ardhi hii itakuwa faida pia kwa watani wangu Wazaramo,” alisema.

Aliwataka wawekezaji hao wa gesi, kupanua huduma zao na kwamba wasiishie mijini, bali waende hadi vijijini kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi huko na ndio wanaotumia kuni na mkaa.

AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI

Aidha, alisema Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji, hivyo wawekezaji wajiamini kwa kuja kuwekeza nchini na kwamba Serikali itawasaidia na kuwaunga mkono.

“Sekta binafsi endeleeni kujiamini, hapa ni mahali salama kwa uwekezaji, tutaendelea kuwahitaji, kuwasaidia na kuwaunga mkono, kikubwa ni kwa sababu Serikali itakusanya kodi,” alisema.

Rais Magufuli alizipongeza sekta binafsi nchini kwa kuamua kuungana na Serikali katika kuwekeza katika gesi asilia. 

Vilevile aliwataka Watanzania wanaotumia mkaa kuanza kutumia gesi ili kupunguza gharama na kulinda afya zao.

“Kwa namna ya pekee naipongeza sekta binafsi kwa kuitikia wito na kuungana na Serikali katika uimarishaji wa nishati nchini kama mlivyomsikia waziri (Waziri wa Nishati, Medard Kalemani) ameeleza nchi yetu inayo kampuni nane zilizopewa leseni ya kuagiza na kusambaza gesi ya mitungi nje ya nchi.

Akizungumzia matumizi ya mkaa, Rais Magufuli alisema Dar es Salaam kwa siku wanatumia magunia 40,000 ya mkaa, hivyo aliwataka Watanzania kubadilika kwa kuanza kutumia gesi.

Kuhusu gharama za gesi, aliwataka wasambazaji kupunguza gharama za kuuza bidhaa hiyo.

Rais Magufuli pia aliipongeza Wizara ya Nishati kwa kuimarisha huduma ya nishati, huku wananchi wengi ikiwemo vijijini wakiunganishiwa umeme.

Alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi mikubwa.

KALEMANI NA MAFANIKIO

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali, sekta ya nishati imepata mafanikio makubwa.

Alisema idadi ya Watanzania wanaotumia gesi ya kupikia imeongezeka kutoka milioni 1 hadi 2.5.

Dk. Kalemani alisema kampuni nane za gesi ya kupikia zimeajiri Watanzania 12,000 na uzalishaji wa umeme kuongezeka kutoka megawati 1,280 hadi kufikia 1,601.

Aidha, Dk. Kalemani alisema Serikali imeanza kukaa na wadau wa sekta ya gesi ili kuangalia utaratibu sahihi utakaowanufaisha walengwa ambao ni watumiaji.

Alisema katika kikao hicho wataangalia ubora, namna miradi hiyo inavyoweza kuwa na mapato makubwa kwa Serikali pamoja na udhibiti wa mazingira.

“Yote haya nimeona nikutaarifu ili uone tulipofikia na uagizaji wa gesi kwa pamoja. Unaweza kudhibiti mapato na nina uhakika Taifa Gas wao wanalipa kodi ipasavyo na wakati huo huo wananchi watumie kitu bora ambacho hakina madhara kwa afya wala mazingira.

“Vikao vyetu tumeshaanza kufanya na tulikaa Machi mwaka huu ili kuangalia namna gani sehemu hizo tunazifanyia kazi ipasavyo,” alisema waziri huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles