Na MWANDISHI WETU-DODOMA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kuelekeza nguvu zake katika kukopesha wananchi wa kawaida wakiwemo wakulima wa pamba wa Kanda ya Ziwa.
Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dodoma, alipokuwa akifungua tawi la saba nchini la TIB (TIB Corporate Bank Limited –TIB-CBL).
“Hivi sasa tunahangaika na mikopo kwa sekta ya pamba. Tunawaomba mwelekee kule,” alisema Majaliwa.
Alisema takwimu zinaonesha ni asilimia 16 tu ya Watanzania wanaotumia mfumo rasmi wa benki hali aliyosema kuwa bado kuna changamoto sekta ya benki katika utoaji wa huduma.
“Mnatakiwa mlifanyie kazi hili. Changamoto ya pili ya sekta ya benki ni tozo na riba kuwa juu zaidi ya mfumuko wa bei. BoT (Benki Kuu) imesaidia sana kwa kupunguza riba zake zinazotumika inapozikopesha benki za biashara na zile za hati fungani,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali ina taarifa kuwa baadhi ya kampuni huandaa taarifa mbili za fedha, moja hupelekwa benki na nyingine hupelekwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Sasa sisi kama Serikali, tukizipata zile zinazopelekwa benki, tutazitumia hizo hizo kukudai kodi kubwa,” alisema.
Najaliwa aliitaka BoT iendelee na utaratibu wa kuzifunga benki zote ambazo hazina tija kama ilivyofanya mwaka jana.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa -CBL, Frank Nyabundege, alisema tawi la benki hiyo la Dodoma limepewa jina la Capital Branch (Tawi la Makao Makuu ya Nchi) likilenga kuwafikia wafanyabiashara wote wa mikoa ya Kanda ya Kati.
Alisema mpaka mwaka jana, TIB-CBL ilikuwa imetoa mikopo inayofika jumla ya Sh bilioni 224.35 kwa taasisi za Serikali.
Alizitaja kuwa ni pamoja na TTCL, MSD, Tanzania Railways Corporation, Tanzania Civil Aviation Authority (TCIA), Urafiki Textile Mills, Camalec na Bariadi District Council.