23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Israel sasa yaingia kati mzozo wa Marekani, Iran

TEHRAN, IRAN

WAKATI mvutano kati ya Marekani na Iran ukizidi kuchukua sura mpya na hata baadhi kujenga hofu kwamba unaweza kuiingiza dunia katika vita kuu ya nne, Jeshi la Israel (IDF) limesema limejipanga kwa kila hali iwapo Iran itaishambulia ama moja kwa moja au kwa njia nyingine.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo hazikutaja chanzo zilizowekwa kwenye mtandao wa The Times of Israel, jeshi hilo limekwishakamilisha hatua nyingi kuhakikisha linaweza kujibu maendeleo yoyote ikiwa ni pamoja na jaribio lolote la Iran kuishambulia Israel, ama kutoka Gaza, Lebanon au Syria.

Taarifa hizi mpya zimekuja siku moja baada ya Iran kusema Marekani imeshindwa kuharibu mifumo yake ya kompyuta inayodhibiti roketi na mitambo yake ya  kurushia makombora.

Juzi Marekani ilisema imefanikiwa kuharibu mifumo hiyo ya kompyuta.

Wajuzi wa masuala ya kidiplomasia, wanasema hatua hiyo ya Israel kujiandaa kijeshi inatokana na Iran kuilenga kutokana na jiografia ya ukaribu wake, lakini kama njia ya kumkomesha adui yake Marekani.

Inaelezwa hatua hiyo ya Iran inatokana na kutambua kuwa Israel imekuwa nguzo ya Marekani  katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya kiteknolojia.

Pengine kwa muktadha huo huo, mwishoni mwa wiki hii Marekani ilimtuma mshauri wake wa masuala ya usalama, John Bolton kwenda Israel na Jumapili alionekana akiwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.

The Times of Israel ikinukuu Channel 12 wameandika kuwa Netanyahu alimshukuru Bolton kwa kusimama pamoja na Israel, lakini pili kwenda kujadili changamoto kubwa wanayokabiliana nayo pamoja Mashariki ya Kati, hasa katika wakati huu aliouita ‘sensitive’.

KAULI YA IRAN

Wakati hali ikiwa hivyo, jana Waziri wa Mawasiliano wa Iran, Mohammad Javad Azari, aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa Marekani ilijaribu kwa nguvu kubwa kuishambulia mifumo ya kompyuta zinazoongoza mifumo ya ulinzi ya Iran, lakini jaribio hilo lilishindikana.

Azari alisema mwaka uliopita Iran ilifanikiwa kuzima majaribio ya mashambulio mtandaoni milioni 33 dhidi ya mifumo yake ya kompyuta.

Mashambulio hayo ameyaita  kuwa ni ugaidi.

Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti mwishoni mwa wiki kuwa nchi hiyo ilifanya mashambulizi ya mtandao dhidi ya mifumo ya makombora ya Iran hata baada ya Rais Donald Trump kusitisha mipango ya kushambulia.

Joto la mvutano kuzidi kupanda baina ya mataifa hayo mawili  linatokana na hatua ya Iran kuidungua ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani wiki iliyopita baada ya kudai kupita katika anga lake na kukaidi kuondoka.

Uamuzi huo ulionekana kupandisha ghadhabu ya Rais Trump ambaye aliyaamuru majeshi ya nchi yake kuishambulia Iran Alhamisi wiki iliyopita kabla ya kubatilisha uamuzi wake huku akisisitiza kuwa ndege yake hiyo ilikuwa inapita katika anga la kimataifa.

Trump alibadili uamuzi wa kulipa kisasi kwa sekunde moja baada ya kuambiwa na majenerali wake kwamba watu 150 wangefariki nchini Iran endapo Marekani ingetekeleza shambulio hilo.

Wakati akitangaza kusitisha  vita hiyo, pengine kama njia ya kuitia hasira Marekani, Iran iliachia mkanda wa video unaoonesha ndege hiyo ikitunguliwa.

Marekani nayo mara moja ilikuwa imeanza kufanya matayarisho ya awali ya kuishambulia Iran.

Pamoja na hayo, Trump mara kadhaa amekaririwa akisema hataki vita, lakini Marekani haitakubali Iran itengeneze silaha za nyuklia.

Uamuzi wa Iran kuidungua ndege ya Marekani unaendeleza sintofahamu baina ya mataifa hayo mawili, hususani katika eneo la mpaka baina ya Ghuba ya Oman na Ghuba ya Uajemi.

Iran tayari imeandika barua Umoja wa Mataifa (UN) ikieleza jinsi inavyochokozwa na Marekani.

Katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Balozi wa Iran wa UN, Majid Takht Ravanchi naye alitoa lugha ile ile inayofanana kimantiki na ya Trump kuwa  Iran haitaki kuingia vitani, lakini ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya maadui.

Tayari Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameonya kuwa vita baina ya mataifa hayo mawili italeta janga ambalo madhara yake hayaelezeki.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres amezitaka pande zinazokinzana kujizuia.

Nchini Marekani, Spika wa Bunge la Wawakilishi kutoka chama cha upinzani cha Democrat, Nancy Pelosi amekwishakaririwa akisema Marekani haina hamu ya vita dhidi ya Iran.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa taifa hilo, na kinara wa kutaka tiketi ya urais kupitia Democrats, Joe Biden, amemkosoa Trump kwa kusema sera zake dhidi ya Iran ni “janga la kujitakia”.

Mzozo wa sasa tayari umesababisha kadhia kadhaa ikiwamo bei ya mafuta katika soko la dunia kupanda kwa asilimia tano.

Zaidi mashirika kadhaa ya ndege yanayopita katika anga la Iran likiwamo lile la United Airlines wiki iliyopita yalisitisha safari zake kwa sababu za kiusalama  baina ya miji ya Newark na Mumbai.

CHANZO CHA MGOGORO

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mgogoro tangu mwaka jana baada ya Rais Trump kujitoa katika mkataba wa kimataifa wa mwaka 2015 uliolenga kumaliza mpango wa nyuklia nchini Iran.

Trump aliamua  kuweka vikwazo baada ya kuona makubaliano hayo yana kasoro.

Uamuzi wa huo wa Marekani ulijibiwa na Iran kwa kuamua kuacha kutekeleza kile ambacho iliahidi kufanya mwanzoni mwa mwezi wa Mei na kutishia kuanza kutengeneza tena nyukilia.

Kumekuwa na mashambulizi dhidi ya meli za mizigo na mafuta katika eneo la Ghuba ya Oman, ambapo Marekani na Saudi Arabia zimeishutumu Iran kuyatekeleza ingawa yenyewe inakanusha.

Marekani imeshaongeza uwepo wa majeshi yake na vifaa vya kivita katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, hali inayoonesha kuwa mzozo huo si wa kuisha leo au kesho.

Habari hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao ya habari ya kimataifa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles