Francis Godwin, Iringa
Serikali wilayani Mufindi mkoani Iringa imesema azimio la dunia la mabadiliko ya tabianchi lililotolewa katika kongamano la wanafunzi lililofanyika nchini Finland watalitumia kama ya kitendea kazi kwao kuona wilaya hiyo inashinda tuzo mbali mbali za uhifadhi wa mazingira .
Akizungumza leo Juni 19, wakati akikabidhiwa azimio hilo kutoka kwa Wanafunzi Stephen Sanga na Mariam Wambura wa shule ya Southern Highlands Mafinga , Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Servi Ndumbalo amesema atalikabidhi kwa Ofisa Mazingira wa wilaya ili kulisoma zaidi kabla ya kulisambaza katika taasisi na shule zote za wilaya hiyo kwa utekelezaji .
Ndumbalo ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mufindi katika hafla hiyo fupi ya kupokea azimio hilo la dunia amesema Wilaya yake imepata heshima kubwa ya kuwakilisha nchi kwenye kongamano hilo na hivyo wanatarajia nafasi hiyo kubwa waliyoipata wanafunzi fursa kwa wilaya na Mkoa wa Iringa katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira .
Amesema kwa kupitia azimio hilo ambalo limegawanyika katika sehemu kuu tatu wao kama wilaya watahakikisha wanatekeleza sehemu ya azimio hilo ambayo imeigusa serikali ili kuona shule zote zinafanikisha utekelezaji wa azimio hilo kwa wakati .
“Tunataka wilaya ya Mufindi kuwa mfano kwa wilaya nyingine nchini katika suala la utuzaji wa mazingira na kwa kupitia azimio hili tutahakikisha tutakwenda hatua kwa hatua kuona tunakidhi vigezo vyote vya ubora katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira na ikiwezekana kushinda tuzo mbali bali za mazingira za ndani na nje ya nchi ,” amesema Ndumbalo.
Amesema maazimio ya kongamano hilo la wanafunzi duniani lililomalizaka nchini Finland watahakikisha wanalitungia kanuni ili kuweza kulitekeleza kwa ufanisi na kila mmoja atapewa majukumu ya kufanya ili kufanikisha utekelezaji wa maazimio hayo .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hamashauri ya Mufindi, Netho Ndilito akishukuru kwa uwakilishi mzuri wa shule hiyo ya Southern Highlands Mafinga katika kongamano hilo amesema heshima ambayo wanafunzi hao wamerejea nayo ni heshima kwa shule hiyo na uongozi wake chini ya Mkurugenzi Mary Mungai na Kitova Mungai na kwao serikali watakuwa bega kwa bega kuona shule nyingine zinapewa elimu ya mazingira .
Ndilito alisema kazi hiyo iliyofanywa na shule hiyo ni kubwa na ndio lengo la serikali kuona mazingira yanaendelea kutunzwa na miti inapandwa kwa wingi ili kuwezesha mradi mkubwa wa umeme unaojengwa kuendelea kuwa endelevu lakini dunia inaendelea kuwa salama bila kukabiliwa na mabadiliko tabianchi .
Amesema Halmashauri yake itahakikisha inatoa ardhi ya wazi kwa shule hiyo ya na shule nyingine za wilaya hiyo ili kupanda miti kama sehemu ya utunzaji wa mazingira na watawatumia wanafunzi hao wawili katika semina mbalimbali kama mabalozi wa mazingira na kuwaelimisha wenzao juu ya mazingira .