MAOFISA wa huduma za dharura nchini Nigeria wamesema watu wasiopungua 30 waliuawa katika mashambulizi matatu ya kujitoa muhanga yaliyofanyika Jumapili Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Washambuliaji wa kujitoa muhanga walijilipua ndani ya ukumbi uliojaa watazamaji wa mechi ya mpira wa miguu katika Kijiji cha Konduga, KM 36 kutoka Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo la Borno.
Bado haijafahamika ni kundi gani lilihusika, lakini waasi wa itikadi kali ya Kiislamu wa Boko Haram wamekuwa wakifanya mashambulizi kama hayo yanayowalenga raia.
Kiongozi wa wanamgambo wa kujihami, Ali Hassan, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba shambulizi lilitokea saa tatu kamili usiku.
Washambuliaji wengine wawili walijiripua katika kibanda cha kunywea chai karibu na ukumbi wa kutazama mechi. Mshambuliaji mmoja alizuiwa na mwenye ukumbi huo kuingia ndani.