AlIYEKUA kiungo mshambuliaji wa Chelsea ya England, Eden Hazard(28)amesema uamuzi wake wa kuihama timu hiyo na kujiunga na Real Madrid ya Hispania, ndio mgumu zaidi kuufanya katika maisha yake ya soka.
Real Madrid katikati ya wiki hii imeingia makubaliano ya mkataba wa miaka mitano na Hazard kwa dau la Pundi milioni 150.
Mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji anatarajia kutambulishwa rasmi na waajiri wake hao wapya Juni 13, baada ya kufanyiwa vipimo vya afya.
Akiichezea Chelsea, aliifungia mabao 110 katika michezo 352, baada ya kujiunga nayo mwaka 2012 akitokea Lile ya Ufaransa 2012.
”Kuondoka kwangu Chelsea ni uamuzi mkubwa na mgumu zaidi katika kipindi changu chote cha kucheza soka”, alisema Hazard.
Aliongezea: Natumaini mtanielewa kwamba nalazimika kutafuta changamoto mpya , ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote anapopambana ili kufikia ndoto yake.
Lazima niweke wazi kitu kimoja, nilifufarisha maisha kipindi chote nilipokuwa Chelsea na hakuna hata siku moja nilifikiria kwamba huenda nikahamia klabu nyingine.”
Mkurugenzi wa Chelsea Marina Granovskaia amekaririwa akisema klabu hiyo haitasahau kamwe kumbukumbu nzuri zilizoachwa na mshambuliaji huyo Stamford Bridge.
”Aliwafurahisha watu wote walioitazama Chelsea ikicheza, tunamshukuru sana Eden Hazard. Ni mchezaji wa kuigwa katika kipindi chake chote alichoichezea Chelsea , ni mtu mzuri wa kushirikiana naye na katika kazi.
”Ijapokuwa ni uchungu sana kumwambia kwaheri Hazard kwani kama klabu ilikuwa bado inamwitaji, lakini tunaheshimu uamuzi wake wa kufuata changamoto mpya katika taifa tofauti na kufuata ndoto yake ya utotoni ya kuichezea Real Madrid.”
Katika misimu saba aliyoichezea Chelsea, Hazard ambaye alibakisha mkataba wa mwaka mmoja , alifanikiwa kushinda Kombe la Ligi, ubingwa wa Ulaya, Kombe la FA na Ligi Kuu.
Pia aliwahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Chelsea mara nne.
Wakati hayo yakijiri, Chelsea itaendelea kutumikia marufuku ya kusajili hadi mwishoni mwa Januari 2020. Hii ina maana kwamba haitaweza kufanya usajili wa kuzina pengo la Hazard.
Awali klabu hiyo ilikatia rufaa uamuzi huo wa Fifa, lakini ikashindwa kabla ya kuwasilisha nyingine katika mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya michezo ambayo inasubiri uamuzi.