27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Uhamiaji yatoa mwezi mmoja kubadili pasipoti

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

IDARA ya Uhamiaji imewataka wananchi wanaofikiria kusafiri nje ya nchi kuhakikisha wanabadilisha hati zao za kusafiria za zamani na kuchukua mpya kabla ya Julai ili kuepuka kuzuiwa katika viwanja vya ndege.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda, alisema mtu anapotoka nje ya nchi ni lazima awe na walau pasipoti yenye uhai wa muda wa miezi sita na kwamba sheria hiyo haijasema mtu huyo awe anakwenda wapi.

 “Kuna nchi nyingine hazikubali wewe uwe na pasipoti ambayo haina muda wa kutosha kwa sababu inategemea wewe kule unaweza kuishi muda gani, tufanye unakwenda sehemu kuishi mwaka mmoja wakati pasipoti yako ina miezi sita.

“Unakuwa huwezi kupata kibali kama unataka kwenda kule, kwahiyo wakaweka ‘standards’ walau iwe na miezi sita ili mtu aweze kusafiri.

“Lakini kwa hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki changamoto ni ndogo kwa sababu mtu anaenda leo na kurudi, huyo anaweza akaitumia, changamoto zaidi kwa watu ambao wanaomba Visa ndiyo tunaona hivyo kwamba nchini nyingi zinaweza kukataa,” alisema Mtanda.

Alipoulizwa kuhusu takwimu za pasipoti za zamani zilizokuwa zimekwishatolewa kabla ya kuanzishwa kwa pasipoti za kielektroniki, alisema upatikanaji wa takwimu hizo si rahisi kwa sababu mfumo wa kumbukumbu zamani haukuwa rafiki.

“Mpaka uanze kuingia kwenye vitabu uanze kujumlisha kwa sababu walikuwa na sehemu tu wanawasainisha, system haikuwa na uwezo wa kurekodi. Siyo kwamba hazipo ila mpaka ukae chini uanze kutengeneza hicho kitu,” alisema Mtanda.

Kuhusu hati mpya za kusafiria zilizotolewa tangu Januari mwaka jana hadi Mei 31, mwaka huu alisema ni 104,362.

Pasipoti hizo ni pamoja na 103,377 za kawaida, 242 za utumishi ambazo hutolewa kwa viongozi waandamizi wa Serikali wakiwamo makatibu wakuu, 741 za diplomasia ambazo hutolewa kwa viongozi kama vile mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali na pasipoti maalumu za diplomasia ambazo hutolewa kwa viongozi wakuu wa nchini.

Awali idara hiyo ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwa tahadhari hiyo inatolewa kwa sababu ya hitaji la kisheria linaloelekeza pasipoti kuwa na angalau uhai wa miezi sita ili mwenye nayo aweze kuomba Visa ya nchi anayokwenda.

“Idara inawasisitiza wenye pasipoti za zamani na wanaokusudia kusafiri nje ya nchi hivi karibuni kuhakikisha wanabadilisha pasipoti zao mapema kabla ya Julai ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wa kurejeshwa katika viwanja vya ndege na vituo vya mipakani wakati wa kutoka nchini,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa matumizi ya hati hizo za zamani yatasitishwa ifikapo Januari 31, mwakani kama ilivyotangazwa tangu kuzinduliwa kwa hati mpya za kusafiria za kielektroniki mapema mwaka jana.

Iliongeza kuwa tayari idara hiyo imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya utoaji wa hati hizo katika mikoa 29 nchini, ofisi za Makao Mkuu ya idara hiyo, afisi kuu za Uhamiaji Zanzibar na balozi 23 za Tanzania zilizopo nje ya nchi ikiwamo Uingereza, Ufaransa na Marekani (Washington DC na New York).

Nyingine ni Canada, Israel, Saudi Arabia (Jeddah na Riyadh), Comoro, Kenya (Nairobi na Mombasa), Ujerumani, Algeria, Italia, Nigeria, Misri, Uholanzi, Ubelgiji, Zambia, India, Malawi, China na Malaysia.

Alisema nchi za Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe zikitarajiwa kufungwa mfumo huo hivi karibuni, huku balozi zilizosalia zikiendelea kufungwa mitambo kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles