Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
SERIKALI imetaja sababu mbalimbali zinazopelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba wa mwaka 2017, ambazo ni upungufu wa walimu, ushiriki hafifu wa wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao na utoro.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara alisema hayo bungeni jana, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbinga, Martin Msuha (CCM).
Akiuliza swali kwa niaba ya Msuha, Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama (CCM) alidai kwamba uhaba wa walimu wa Hisabati na Sayansi umeathiri matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 Wilayani Mbinga.
Mbunge huyo alihoji Serikali ina mpango gani wa kupeleka walimu wa masomo hayo wilayani humo.
Akijibu swali hilo, Waitara alisema zipo sababu za kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba wa mwaka 2017 Wilaya ya Mbinga ikiwemo upungufu wa walimu, utoro na ushiriki hafifu wa wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao.
Naibu Waziri huyo alisema walimu wa shule wanaoajiriwa wanaweza kufundisha masomo yote yaani na Sayansi na Hisabati.
“Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga walimu kwenye halmashauri hasa zenye upungufu wa walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha,”alisema Waitara.