RIO DE JANEIRO, Brazil
MAHAKAMA Kuu ya hapa imesema mwanamume aliyemshambulia Rais Jair Bolsonaro Septemba mwaka jana wakati wa kampeini ana ugonjwa wa akili na hivyo hawezi kufungwa.
Jaji Bruno Savino, alisema juzi kwamba Adélio Bispo de Oliveira wakati akifanya tukio hilo, alikuwa hawafahamu alichokuwa anakifanya kutokana na matatizo yake ya akili na hivyo hawezi kufungwa kutokana na kosa hilo.
Awali, Rais Bolsonaro, ambaye alihitaji kufanyiwa upasuaji baada ya tukio hilo alikuwa akiamini ni masuala ya msukumo wa siasa.
Hata hivyo baadaye polisi walisema watamfanyia mwanamume huo uchunguzi kuona kama alikuwa na matatizo ya akili, baada ya kuwaeleza kwamba alifanya kitendo hicho kwa maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Akitoa hukumu hiyo juzi, Jaji Savino alisema alifikia uamuzi huo kutokana na ripoti iliyowasilishwa na wakili aliyekuwa akimtetea De Oliveira.
Katika tukio hilo, Rais Bolsonaro (64), alinusurika kifo baada ya kupata majeraha makubwa baada ya kushambuliwa maeneo ya tumbo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Minas Gerais Septemba mwaka jana.
Mwanasiasa huyo mwenye mrengo wa kulia alilazimika kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kutokana na majeraha hayo ambayo yalisababisha hata mfumo wake wa kumeng’enya chakula kushindwa kufanya kazi hadi akawekewa mfuko maalum tumboni kabla ya kutolewa Januari mwaka huu.
Rais Bolsonaro, ambaye alikabidhiwa madaraka ya nchi Januari mwaka huu ni mwanasiasa mtata ambaye wachambuzi wa masuala ya siasa wanamfananisha na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Adélio Bispo de Oliveira ni mfuasi wa sera zamrengo wa kushoto ambaye amekuwa akipaza sauti kumshutumu Rais Bolsonaro, akitumia njia ya ujumbe wa Facebook kunadi sera zake.