MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
RAIS wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo, ametua nchini kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam akitokea nchini Afrika Kusini kuelekea nchini kwake.
Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola jana uwanjani hapo, baada ya kupokewa Rais Farmajo alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kukuza uchumi na kuwa na uongozi imara katika nchi yake.
“Nina furaha kuingia Tanzania japo kwa dharura, kwa kuwa nchi hii ni rafiki na Somalia, naomba mpelekee ujumbe huu Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, na pia mpe pongezi kwa kukuza uchumi,” alisema Rais Farmajo.
Rais huyo wa Somalia, alitua nchini kwa ajili ya ndege anayoitumia kuwekwa mafuta, pia alimwomba Rais Magufuli, nchi yake iweze kupata idadi kamili ya wazuiwa na wafungwa wote ambao wana kesi zinazohusiana na uhamiaji haramu waliopo magerezani hapa nchini, ili Serikali ya Somalia iweze kuwasafirisha kwa mujibu wa sheria.
“Serikali ya Somalia inatambua kuwa na uhusiano madhubuti na Tanzania, Somalia ipo tayari kufanya utaratibu wa kisheria ili kuweza kuwarudisha nyumbani wafungwa wote ambao wanakesi zinazohusiana na uhamiaji,” alisema Rais Farmajo.
Pia Rais Farmajo ameishukuru Tanzania, kuwapa mazingira mazuri ya biashara, wafanyabiashara na wawekezaji wenye asili ya Somalia waliopo nchini.
Rais Farmajo aliwasili saa 8:38 mchana na kufanya mazungumzo na Waziri Lugola kwa muda wa dakika 30 na baadaye aliondoka nchini kuelekea Somalia.