MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA Mbunge wa Singida Kaskazini kabla ya kuhamia Chadema, Lazaro Nyalandu, anashikiliwa na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Singida Mjini kwa kosa ambalo bado halijafahamika.
Akizungumza na gazeti hili jana jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mrema, alisema bado hawajajua sababu za kukamatwa kwa mwanasiasa huyo.
Alisema Nyalandu alivamiwa na watu waliokuwa na silaha wakati akiwa katika kikao na makada wa Chadema pamoja na aliyekuwa mgombea wa chama hicho katika Jimbo la Singida Kaskazini, Daniel Jumbe na Mwenyekiti wa Kata ya Itaja, aliyefahamika kwa jina moja la Samson.
“Wakiwa kwenye kikao, watu wasiojulikana wakiwa na silaha walivamia kikao hicho na kuondoka na Nyalandu na viongozi hao na hawakusema sababu za kukamatwa,” alisema Mrema.
Alisema katika hatua ya awali tayari chama kimewatuma mawakili wake ili kushuguhulikia suala hilo.
Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetberth Njewike, alikiri kuwapo tukio hilo na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na Takukuru.
“Ni kweli anashikiliwa na taasisi hiyo, taarifa zaidi mtapewa na Takukuru wenyewe,” alisema kamanda huyo.