26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya FBME yawekwa chini ya uangalizi

FBME
FBME

NA MWANDISHI WETU

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) jana ilitangaza kuchukua usimamizi wa Benki ya FBME Tanzania, MTANZANIA Jumamosi linaripoti.

Hatua hiyo imechukuliwa kuanzia juzi Alhamisi kutokana na kashfa zilizoikumba benki hiyo inayomilikiwa na raia wa Lebanon.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa uamuzi huo umetokana na Benki Kuu ya Cyprus (CBC) kuchukua uendeshaji tawi la FBME Ltd nchini Cyprus, kufuatia taarifa za Mtandao wa Kupambana na Uhalifu wa Kifedha wa Marekani (FinCEN), kuihusisha na uhalifu wa kifedha.

“Kutokana na athari zitakazosababishwa na uamuzi huo katika mfumo wa kibenki wa Tanzania, umma unajulishwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania, kufuatana na masharti ya kifungu namba 56 (1)(g)(iii) cha Sheria ya Kibenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, imechukua rasmi usimamizi wa Benki ya FBME Tanzania kuanzia Julai 24, 2014,” taarifa hiyo iliyopatikana katika mtandao wa BoT ilisema.

Taarifa ya BoT iliendelea kueleza kuwa, lengo la uamuzi wake huo ni kuhakikisha akiba za wateja zinakuwa salama kwa mujibu wa mfumo mzima wa kibenki.

“Wakati benki hiyo ikiwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania, umma unafahamishwa zaidi kuwa operesheni za benki hiyo zitaendelea kama kawaida,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya BoT inakuja siku chache tu baada ya awali kukanusha minong’ono iliyosambazwa mitandaoni kuwa imechukua udhibiti wa benki hiyo ya Lebanon.

Taarifa hiyo ya awali ya Julai 20 iliyotolewa na Idara ya Uhusiano na Itifaki ya BOT, ilisema: “ Benki Kuu ya Tanzania inapenda kukanusha habari zinazosambazwa na mitandao kuwa kesho Jumatatu (Julai 21) Benki ya FBME itafungwa na shughuli zote za benki hiyo zitakuwa chini ya Benki Kuu”.

“Habari hizi si za kweli na kwamba benki hiyo haipo chini ya usimamizi wa BOT na itaendelea kutoa huduma kama kawaida,” taarifa hiyo fupi ilisema.

Ukiachana na taarifa hizo za BOT, awali wiki iliyopita CBC ilichukua uendeshaji wa benki hiyo siku moja tu baada ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuifuta benki hiyo katika mfumo wake wa fedha.

“Benki Kuu ya Cyprus (CBC) imetangaza kuwa chini ya mamlaka halali iliyo nayo kisheria, imechukua kuanzia leo (Julai 18) uendeshaji wa shughuli za tawi la Benki ya FBME Ltd nchini Cyprus,” CBC ilisema katika tovuti yake.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa FBME, Ayoub-Farid Saab, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ni yeye ndiye aliyeiomba Cyprus kuchukua hatua hiyo ili kuisafisha na tuhuma alizoziita zisizo na msingi.

“Tunaendesha shughuli safi katika kisiwa hiki,” alisema.

Siku moja kabla ya Cyprus kuchukua uamuzi huo, Wizara ya Fedha ya Marekani iliituhumu FBME, kuwezesha shughuli za kifedha kwa makundi ya kihalifu na kigaidi ikiwamo Hezbollah la Lebanon, ambalo imeliorodhesha kama kundi la kigaidi.

“FBME inafahamika kwa mfumo wake dhaifu wa Udhibiti wa Uhalifu wa Kifedha (AML), unaotoa nafasi kwa shughuli chafu katika dunia ya uhalifu,” Mkurugenzi wa Mtandao wa Kudhibiti Uhalifu wa Kifedha katika Wizara ya Fedha ya Marekani, Jennifer Shasky Calvery, alisema katika taarifa yake Alhamisi iliyopita.

“Hatua ya leo ya kufunga shughuli za FBME kutoka mfumo wa kifedha wa Marekani ni ya lazima ya kuharibu harakati hizo chafu za benki hiyo,” alisema.

FBME, ambayo zamani ilijulikana kama Benki ya Shirikisho ya Mashariki ya Kati, ikiwa imezinduliwa nchini Cyprus mwaka 1982 ni sehemu ya Benki ya Shirikisho ya Lebanon, ambayo inaendesha pia shughuli nchini Tanzania kwa mujibu wa tovuti yake.

Kwa mujibu wa tovuti ya Benki ya Shirikisho ya Lebanon, kampuni hizo mbili ni sehemu ya Saab Financial Group na inamilikiwa na ndugu wawili; Ayoub-Farid Saab na kaka yake Fadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles