RAYMOND MINJA, IRINGA
Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa,Joseph Lyata, ametoa siku Tano kwa kikundi cha wafanyabiashara wa minadani (WAMMA) kuitisha uchaguzi na wa viongozi wapya ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima.
Uamuzi huo wa Naibu Meya umekuja mara baada ya viongozi wa kikundi hicho kijiuzulu nafasi zao jana Mei 24 .
Akizungumza na wanachama hao leo Mei 25, kwenye mkutano aliouitisha amesema mara baada ya kusikiliza pande zote mbili viongozi na wanachama ni vema kufanya uchaguzi wa viongozi wapya ili kuendesha kikundi hicho.
“Ndugu zangu sasa tumefikia sehemu nzuri tumefanya mazungumzo kwa
amani bila hata ya kuwepo kwa polisi na viongozi wamekiri mapungufu
yao na katika hali ya kawaida hakuna binadamu asiyekuwa na mapungufu
na hata nyie wanachama mna mapungufu yenu hivyo basi ndani ya siku
tano tumekubaliana hapa tuitishe mkutano mkuu na tufanye uchaguzi wa
viongozi wetu maana hawa waliopo hawapo kisheria “ amesema lyata
Amesema wafanyabiashara wadogo wadogo ni watu muhimu sana kwenye nchi hii na ndiyo maana Rais Magufuli amekuwa akiwatetea na kuwapigania wafanyabiashara wadogo hasa machinga na ndiyo maana akatoa maelekezo kwa viongozi aliowateuwa kuwapigania
wafanyabiashara hao ili wasibughudhiwe na mtu yoyote .
“Ndugu zangu nyie ni watu muhimu sana mmekuwa mkifanya kazi nzuri na
ndiyo maana nchi yetu inasonga mbele kwani sote tunategemeana na ndiyo
maana leo tumekuja hapa pamoja na watendaji wa manispaa ili kufanya
kikundi hiki kisife bali kiendelea na baadae hata kuja kuwa benki kama
vikundi vingine vilivyoanza.