27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Nilipata ulemavu nikiwa mdogo, ndugu zangu wakaanza kunilaza stoo

Na AVELINE KITOMARY 

ULEMAVU ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au ya kiakili, inaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu. Hali hii humpunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Tafiti zinaonesha kuwa takribani asilimia 10 ya idadi ya watu wote duniani ni walemavu wanaojikimu maisha yao kwa kuombaomba katika miji hasa barani Afrika, lakini madhila wanayopata hayazingatiwi. 

Hali ya mtu kuwa na ulemavu huambatana na unyanyapaa unaotokana na mila zilizopitwa na wakati.

Baadhi ya walemavu wamekuwa wakifungiwa majumbani na familia zao kwa sababu wanaonekana kama ni jambo la ajabu mbele za watu na hata wengine kuwaona ni laana kuwapo ndani ya familia. 

Hali hii kwa kiasi kikubwa imechangia asilimia kubwa ya walemavu kuwa tegemezi kwa sababu ya kunyimwa fursa ya kupata elimu na haki zao zingine za msingi.

Huku ni kwenda kinyume na haki za msingi za binadamu na hasa ukizingatia kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na wanastahili kupata haki sawa bila kujali rangi, kabila, jinsi na dini.

Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha Desemba 20, mwaka 1948 ulipitisha Azimio Na. 27 (a) (III) linaloeleza kwamba binadamu wote wamezaliwa huru wakiwa sawa katika haki na kustahili heshima.

Awali, utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini haukuwa na sera maalumu bali ulikuwa ukifanywa kwa kadri matatizo yalivyojitokeza na maelekezo mbalilmbali ya Serikali na chama tawala (kwa mfano Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha).

Kutangazwa kwa mwaka wa 1981 kuwa ni mwaka wa Kimataifa wa Watu Wenye Ulemavu, kulileta vuguvugu lililoifanya Serikali kutayarisha miongozo na kupanga mikakati ya utoaji huduma kwa walemavu. 

Juhudi bado zinahitajika katika kusimamia sheria zilizowekwa kwaajili ya watu wenye ulemavu ikiwapo ile ya ajira.

Aisha Mbaruku ni miongoni mwa watu ambao walipata ulemavu baada ya kuugua. Binti huyu amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi maishani kutokana na ulemavu alionao. 

Aisha ni mzaliwa wa Ruvu Station, mkoani Pwani ambaye kwa sasa anaishi hapa jijini. 

Binti huyu anasema hajawahi kubahatika kumuona mama yake wala baba yake kwa sababu mama yake alifariki sekunde chache mara baada ya yeye kuzaliwa, huku baba yake akiwa hajulikani alipo ingawa anaambiwa ni mzaliwa wa Kigoma. 

“Nilitamani niwaone wazazi wangu, lakini sijafanikiwa, niliambiwa mama alifariki muda mchache baada ya mimi kuzaliwa, nafkiri ilikuwa bahati mbaya kwangu,” anasema Aisha.

CHANZO CHA KUPATA ULEMAVU 

Aisha anasema mara baada ya mama yake kufariki alilelewa na bibi na mjomba wake.

Anasema hakuzaliwa akiwa mlemavu bali alikutwa na hali hiyo miaka 6 au 7 baadae.

“Bibi alinisimulia kuwa siku moja jioni nilianza kuugua homa na wakati huo huo mguu mmoja ukaanza kuuma, bibi hakuweza kunipeleka hospitali mapema kwa sababu hakuwa na uwezo kifedha. 

“Kutokana na maumivu ya mguu niliyokuwa nayo,  alikuwa akinipeleka kufanya mazoezi ya kutembea lakini hali haikubadilika ;lakini pia sikupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” anasema Aisha na kuongeza:  

“Baada ya muda mfupi, miguu yote ikawa inauma na tangu hapo sikuweza kutembea wala kucheza na wenzangu, nilibaki nyumbani tu. Sikufurahia hali hiyo lakini sikuwa na  la kufanya.”

CHANGAMOTO ZA KUPATA ELIMU 

Anasema baadae alienda kuishi kwa mjomba wake ambaye alitamani kumsomesha lakini alishindwa kutokana na kukosa shule itakayoendana na hali yake hivyo, akaanza kusoma elimu ya dini (Madrasa).

“Siku moja alikuja mlemavu mmoja akamwambia mjomba shule ya walemavua ipo, akanichukulia fomu hapo ndipo nilipoanza darasa la kwanza nikiwa na umri mkubwa,” anasema Aisha.

Aisha anasema alisoma darasa la kwanza hadi la tatu lakini kwa bahati mbaya mjomba wake alifariki.

“Baada ya mjomba kufariki bibi alirudi Pwani na kuniacha na watoto wa mjomba, haikuchukua muda mrefu bibi naye akafariki, ingawa mjomba aliacha wosia kuwa akifa niendelee kusomeshwa lakini hali ilibadilika.

“Watoto wa mjomba walinihamishia kwenye chumba ambacho kilikuwa stoo, haikuwa na miundombinu rafiki kwangu, wakaniambia hawawezi tena kunilipia ada hivyo sitaendelea na masomo,” anasema Aisha.

Anasema aliwaelewa walezi wa shuleni kuhusu kutaka kuachishwa shule hata hivyo, walimwambia watamsomesha hadi atakapomaliza darasa la saba.

“Nilimaliza darasa la saba, Baada ya kumaliza nilirudi nyumbani sikufanikiwa kufaulu. 

NDUGU WALIVYOMNYANYASA 

Mtazamo wa ndugu kutokana na hali ya Aisha ilikuwa tofauti na wengine, walimwambia amekuwa mlemavu kutokana na mama yake kuwa mlemavu huku wengine wakidai ni imani za kishirikina. 

Safari ya Aisha bila bibi yake wala mjomba ilikuwa ngumu kutokana na watoto wa mjomba kuanza kumyanyasa kwa kumfukuza katika nyumba yao huku akiwa hajui pa kwenda.

Anasimulia: “Licha ya mjomba kusema niangaliwe lakini watoto wake walianza kuninyanyasa, walinitoa kwenye chumba nilichokuwa ninakaa wakanihamishia stoo. 

“Kuna wakati wakaamua kunitaka niondoke nisiishi tena kwenye nyumba yao, nikaondoka nikawa nalala nje, waliuza baiskeli yangu ambayo ilikuwa inanisaidia kutembea, nilienda kuwashtaki serikali za mtaa lakini hawakunisaidia.

“Kuna siku nilienda kuwadai wakanipiga, wasamaria wema wakanisaidia, niliumwa nikaenda hospitali nikapewa dawa za maumivu.

“Ndugu zangu wote hakuna anayenijali wala kunitafuta, nina miaka mitatu sasa sijamwona ndugu yeyote wote wamenitenga.”

ALIVYOSAIDIWA 

Aisha anasema baada ya watu waliowazunguka kuona mateso anayoyapata, wakaamua kumsaidia kwa kumpa hifadhi. 

“Kuna dada nilikuwa nimezoeana naye kwao ni Zanzibar, alinichukua na kunipeleka huko lakini baada ya muda mfupi niliaanza kuumwa, alinipeleka hospitali lakini ugonjwa haukuonekana.

“Alinirudisha Dar es Salaam nikapelekwa hospitali na msikitini, nilivyorudi afya yangu iliimarika,” anasema Aisha.

Akielezea kwa huzuni, anasema baada ya kukaa mtaani alikutana na mama mmoja anayemtambulisha kwa jina moja la Sabrina, anaishi Yombo. Mama huyo alimwonea huruma akamchukua ili akakae naye kwake.

“Niliishi kwa huyo mama miezi mitatu lakini baadae nikawa sipatani na watoto wake, kwani walikuwa wakinidharau nikaondoka kwenda kuishi mtaani. 

“Siku moja nilikuwa naenda Kariakoo, nikakutana na rafiki yangu anaitwa Mariam ambaye pia ni mlemavu na ni mfanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo, akanichukua nikaenda kuishi naye.

“Tulikuwa tunaishi na mama yake, lakini kwa bahati mbaya yake alifariki, hali ya maisha ikawa ngumu kwetu hivyo rafiki yangu akanishauri niende Machinga Complex hapo nitapata msaada,” anaeleza Aisha.

HALI YAKE YA SASA 

Kwa sasa anaishi maeneo ya Machinga Complex katika chumba kimoja na rafiki yake lakini maisha kwake bado ni magumu. 

Aisha anaeleza kuwa  amejiunga na Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu Dar es Salaam (UWAWADA), kutegemea kupata msaada kutoka hapo.

Anatamani kuwa mfanyabiashara wa vinywaji lakini mtaji umekuwa mdogo hivyo anashindwa kufanikisha ndoto yake hiyo. 

“Natamani kuwa mfanyabiashara mkubwa na naamini nitafanikiwa, nahitaji msaada wa mtaji ili niweze kukua kiuchumi,” anasema.

Anasema biashara ndio njia pekee itakayomfanya ajikwamue kutoka hapo alipo. Anatoa namba kwa yeyote atayeguswa kumsaidia ampigie kupitia namba 0717 436 112.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles