NA ALLAN VICENT
JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia Salma Hassan, mkazi wa Kata ya Malolo katika Manispaa ya Tabora kwa tuhuma za kujeruhi kwa kumchoma moto mapajani mtoto mdogo Johari (3) aache tabia ya kukojoa kitandani.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Emanuel Nley alisema mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma hizo na ikibainika kahusika katika unyanyasaji huo atafikishwa mahakamani.
Alisema awali ndugu wa karibu wa mtoto huyo walikuwa hawataki habari hizo zijulikane hivyo wakakaa kimya lakini polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ndiyo maana mtuhumiwa huyo ameweza kukamatwa.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni jirani na familia hiyo (ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini) alieleza kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kitendo hicho cha kinyama mara kwa mara.
Alidai aligundua tatizo hilo Mei 5 mwaka huu baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumbeba mtoto huyo ambaye alikuwa akilalamika kwa maumivu makali na alipomhoji ndipo akagundua kufanyiwakitendo hicho.
“Nilipita nyumbani kwao nikambeba mtoto huyo lakini alikuwa analalamika kuwa anaumia kwenye mapaja.
“Nilipomuuliza amefanya nini akaeleza kuwa ana vidonda pajani kwamba alichomwa moto na shangazi yake akome kukojoa kitandani,” alidai.
Alieleza kuwa mtoto huyo alidai kuwa shangazi yake alimchoma moto mapajani aache tabia ya kukojoa kitandani.
Alisema hali hiyo ilimfanya kwenda kutoa taarifa polisi.
Shuhuda huyo aliomba hatua za sheria zichukuliwe kukomesha vitendo vya namna hiyo ambavyo ni vya kinyama na ukatili mkubwa kwa watoto wadogo na hasa ikichukuliwa kuwa vinafanywa na kinamama wasiojali.