Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limesema limepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa za kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Media na mlezi wa Timu ya Taifa ya Vijana U17 (Serengeti Boys) Dk. Reginald Mengi.
Dk. Mengi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Mei 2, nchini Dubai alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katika taarifa ya Rais wa TFF, Wallace Karia, iliyotolewa leo na Afisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo leo imesema Dk. Mengi alikuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu ambao bado ulikuwa unamuhitaji.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za msiba wa mlezi wetu wa Serengeti Boys, sote ni mashahidi kwa namna alivyojitolea katika mpira wa miguu kuanzia ngazi ya klabu hadi timu za Taifa hakika mchango wake bado unahitajika kwa niaba ya TFF natoa pole kwa familia yake, makampuni ya IPP, ndugu na wanafamilia ya mpira wa miguu nchini kote,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kwamba Dk. Mengi alikuwa mlezi wa Serengeti boys ambapo mara ya mwisho alikuwa na timu hiyo iliposhiriki katika fainali za Afrika za Vijana U17 (AFCON) zilizofanyika nchini na kumalizika Aprili 28 mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.