KHARTOUM, SUDAN
WAANDAMANAJI nchini hapa wametoa wito wa kufanyika maandamano makubwa leo wakisisitiza kuwa jeshi halina nia thabiti ya kukabidhi madaraka kwa raia karibu wiki tatu baada ya kuuondoa madarakani utawala wa Omar al-Bashir.
Wito huo unakuja wakati hali ya wasiwasi ikiongezeka kuhusu muundo wa Baraza jipya la pamoja kati ya raia na jeshi litakaloiongoza Sudan, wakati waandamanaji wakiimarisha vizuizi nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.
Pande hizo mbili zina mambo mengi yanayokinzana kuhusu uwakilishi katika baraza hilo jipya ambalo linatarajiwa kuchukua nafasi ya lile la kijeshi lililochukua madaraka baada ya kuondolewa kwa al-Bashir Aprili 11, mwaka huu kufuatia maandamano makubwa ya umma kupinga utawala wake wa miongo mitatu.
Jeshi limekuwa likitaka baraza lenye wajumbe 10 ikiwa ni pamoja na wawakilishi saba wa jeshi na raia watatu.
Lakini waandamanaji wanataka wingi wa raia katika baraza litakalokuwa na wajumbe 15, ambapo wawakilishi wa jeshi wakitakiwa saba.
Kutokubaliana kumesababisha Muungano kwa ajili ya Uhuru na Mabadiliko kutangaza maandamano ya watu milioni moja leo kusisitiza dai lao kuu, ambalo ni “utawala wa kiraia”.
“Baraza la kijeshi halina nia thabiti juu ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa raia.
“Baraza la kijeshi linasisitiza baraza la pamoja liongozwe na wanajeshi likiwa tu na wawakilishi wachache wa kiraia,” alisema Mohamed Naji al-Assam, kiongozi wa Chama cha Wanataaluma wa Sudan (SPA) kilichoongoza maandamano hayo na kuongeza kuwa jeshi limekuwa linataka kupanua madaraka yake kila siku.
“Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono uchaguzi wa watu wa Sudan.
“Tunahisi kutokana na vitendo hivi vya Baraza la Mpito la Kijeshi hadi wakati huu, halina nia ya dhati kuhamisha madaraka kwa raia, licha ya ahadi wakati lilipoingia madarakani, lilipodai limeingia madarakani kutokana na madai ya umma na kuahidi litahamisha mamlaka kwa raia haraka iwezekanavyo.
“Lakini sasa tunachoshuhudia ni muda unapita wakati madaraka ya baraza la kijeshi yanaongezeka na hii ni hatari kwa mapinduzi ya Sudan,” alisisitiza.
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi habari, Madani Abbas Madani, kiongozi mwingine wa maandamano, amelishutumu baraza la kijeshi kwa kutumia lugha ya kuongeza mivutano ambayo haishawishi ushirikiano.
Taarifa zao zimekuja baada ya jenerali mwandamizi wa jeshi la Sudan kutangaza chombo hicho kipya kitaongozwa na kiongozi wa sasa wa kijeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.