AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, imempandisha kizimbani Justin Makoba(27) kwa shtaka la kukutwa na sare ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kinyume cha sheria.
Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Adelf Sachore, Mwendesha Mashtaka wa Jamuhuri, Grace Mwanga alidai Aprili 2, mwaka huu eneo la Upanga Fire, Wilaya ya Ilala mtuhumiwa alikutwa na suruali tatu,fulana tatu, koti na kofia mali ya jeshi hilo, huku akizipata kwa njia isiyohalali.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo, huku upande wa Jamuhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.
Hakimu Sachore, alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka katika taasisi inayotambulika ambao watatoa bondi ya Sh millioni 4 kwa kila mmoja.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande mpaka kesi yake itakaposomwa tena Mei 14. mwaka huu.
Wakati huo huo,mahakama imempandisha kizimbani Husen Mboneka, Mkazi wa Tabata Segerea kwa shtaka la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 54.91.
Akisoma shtaka hilo,Mwendesha mashtaka wa Serikali Grace Mwanga alidai mbele ya Hakimu Sachore kuwa Machi 28, mwaka huu eneo la Tabata Segerea Wilaya ya Ilala mshtakiwa alikutwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya huku akijua ni kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikanusha kutenda tuhuma hizo,upande wa Jamuhuri ulisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena .
Mshtakiwa alishindwa kutimiza vigezo vya dhamana na kurudishwa rumande mpaka kesi yake itakaposomwa tena Mei 14 mwaka huu.