- TMA yatoa tahadhari, baadhi ya nchi nazo kuathirika
ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa uwepo wa mvua kubwa katika siku tano zijazo, kutokana na mabadiliko ya kitropoki.
Akizungunza na MTANZANIA jana, Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri TMA, Samwel Mbuya, alisema hali hiyo inatokana na mgandamizo mdogo wa hewa katika pwani ya visiwa vya Madagascar.
“Katika taarifa yetu inaonesha kuwa leo (jana) na siku tano zijazo kutakuwa na mgandamizo mdogo wa hewa kwenye Bahari ya Hindi, kaskazini mwa visiwa vya Madagascar, hali inayoongeza mawingu ya mvua katika maeneo mengi ya pwani ya bahari hiyo na maeneo kadhaa ya nchi.
“Tunatoa angalizo la uwezekano wa kuwepo kwa mvua nyingi na kuongezeka kwa ukubwa wa mawimbi ya bahari kutokana na hali hiyo. Lakini pia katika maeneo ya pwani kutakuwa na uwezekano wa kuwa na joto kali pia kutokana na hali hiyo,” alisema.
Alisema bado hawajatoa tahadhari yoyote kuhusu uwezekano wa kutokea kwa kimbunga katika eneo la Bahari ya Hindi kwa sasa.
Mbuya alizungumza hayo alipoulizwa kuhusu tahadhari ya kimbunga Kenneth iliyotolewa kupitia akaunti ya facebook ya hurricane/typhoon/cyclone alerts ikieleza kuwa katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mfumo wa kitropiki, kutatokea kimbunga kilichopewa jina la #CycloneKenneth kati ya leo hadi Aprili 30.
Taarifa hiyo ilitoa tahadhari kwa watu wote waishio kusini mwa Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kufuatilia kimbunga hicho cha kitropiki kinachotarajiwa kutokea upande wa kusini magharini mwa Bahari ya Hindi kuanzia leo.
“Baada ya uchambuzi wa hivi karibuni, Aprili 21, 2019 (Jumapili ya Pasaka), upo uwezekano mkubwa wa kutokea kimbunga hicho #Kenneth katika eneo la mpaka wa Tanzania na Msumbiji, hasa ifikapo Aprili 26, 2019.
“Kwa hiyo, watu wote wa kusini mwa Tanzania na Msumbiji wa kaskazini wanapaswa kuanza kufikiri kuhusu kufanya mipango ikiwa ni pamoja na kupata makazi ya dharura, kupanga mipango ya kufanya uokoaji kwenye pwani karibu na mpaka wa Tanzania/Msumbiji.
“Pia wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na athari zitokanazo na maji (mafuriko ya pwani, kuongezeka kwa dhoruba ikiwa ni pamoja na mawimbi makubwa, mafuriko ya nchi kutoka kwenye mawimbi makali vya kitropiki) na athari za upepo ikiwa ni pamoja na upepo hatari wa cyclone unaokwenda kwa kasi ya kilometa 89-130 kwa saa,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia ilitoa tahadhari kwa watu wote kwenye visiwa vya Shelisheli, Comoro, Mayotte na Madagascar kuchukua tahadhari na kufuatilia kwa karibu hali hiyo kuanzia leo hado Aprili 30, kwa kuwa upo uwezekano wa kupata athari zisizo za moja kwa moja ikiwa ni pamoja na ongezeko la ukubwa wa mawimbi.
Ilieleza kuwa kutakuwa na mawimbi makubwa na upepo mkali wa kitropiki, hivyo ni vyema watu wakichukua tahadhari kaskazini magharibi ya Visiwa vya Comoro na Mayotte.
“Iwapo kimbunga Kenneth kitatokea wiki hii kama inavyotarajiwa, hali ya kimbunga hicho itaweza kuleta athari pia kwenye visiwa vyote vya Shelisheli hadi visiwa vya Comoro, hivyo ni vyema watu wa maeneo hayo wakichukua pia tahadhari,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa rasmi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa iliyotolewa juzi, ilitoa angalizo kuwa kutakuwa na vipindi vifupi vya upepo mkali unaofikia kilometa 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili katika baadhi ya maeneo ya pwani, katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Ilieleza pia kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa hiyo ya TMA inaeleza pia kuwa upepo wa pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya km 40 kwa saa kutoka kusini kwa pwani yote, hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa na matazamio kwa siku ya leo ni kuendelea kwa mvua katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani.